Habari
Waziri Masauni awatia moyo wadau wanaofanya shughuli za kutunza mazingira
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni amesema Serikali inatambua na kuthamini mchango wa wadau hususan vijana katika jitihada za utunzaji na usafi wa mazingira nchini.
Amesema hayo alipokutana na vijana Bi. Irene Ombeni na Bw. Switbert Vedasto wanaojitolea kufanya usafi wilayani Kigamboni mkoani Dar es Salaam na Bi. Upendo Lyimo ambaye na mshindi wa tuzo ya Umoja wa Mataifa ya Mazingira aliowaalika kumtembelea bungeni jijini Dodoma leo Novemba 03, 2026.
Akizungumza mara baada ya kufanya mazungumzo na vijana hao katika viwanja vya Bunge, Mhandisi Masauni alisema vijana hao wanafanya kazi nzuri ya kuisadia nchi katika utunzaji wa mazingira.
“Nimemuona Irene kwenye mitandao ya kijamii kwakweli anafanya kazi nzuri ya usafi kwenye mitaro na baada ya kumuona nimevutiwa na shughuli zake, ni kijana mwenye moyo wa kuigwa na vijana wengine na kuna umuhimu kwetu sisi Serikali kumtambua,” alisema.
Masauni alitoa wito kwa vijana wengine kuona umuhimu wa kuwa wazalendo na kujitoa bila kutegemea nini utalipwa bali utaona matunda yake katika siku za usoni akitolea mfano wa fursa ambazo zinapatikana kupitia sekta ya mazingira.
Kutokana na mchango wake kwa jamii, Mhandisi Masauni alimuahidi kumuwezesha kusoma hadi elimu ya juu ili aweze kufikia malengo yake ya kuisaidia jamii hususan katika utunzaji wa mazingira.
Kwa upande mwingine Waziri Masauni alimpongeza Bi. Pendo ambaye alitwaa tuzo ya ubunifu wa namna ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi akimulezea kuwa ameiheshimisha nchi.
Kutokana na mchango wa mwanamazingira huyo, Masauni alisema ni wakati sasa wa kumualika katika Ofisi ya Makamu wa Rais kwa ajili ya kuwasilisha wasilisho lake la ubunifu wa ufumbuzi wa athari za mabadiliko ya tabianchi.
Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI) Prof. Riziki Shemdoe aliwaomba wakuu wa mikoa na wilaya hasa Kigamboni kutoa ushirikiano kwa vijana wanaojitolea kufanya usafi.
Nae Bi. Irene alisema kuwa anatamani vijana wengine waige anavyofanya shughuli za usafi kwa kujitolea ndio maana anatumia mitandao ili kuwahamasisha.



