Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe Dkt. Selemani Jafo amelipongeza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira NEMC kwa usimamizi mzuri wa Sheria ya Mazingira katika mradi wa kufua Umeme wa Bwawa la Mwalimu Nyerere (JNHPP).
Ametoa pongezi hizo wakati wa ziara ya kukagua eneo la mradi huo kwa lengo la kujiridhisha na hatua za ujenzi zilipofikia sambamba na suala la utunzaji na uhifadhi wa mazingira.
”Mradi huu ni mkubwa wenye shughuli kubwa na nyingi zinazozalisha taka za kila aina na idadi ya watu takribani 12,000, hutegemei kukuta mazingira nadhifu kama haya, hizi zote ni juhudi za Baraza la Mazingira ambalo lilipiga kambi kabisa hapa kuhakikisha Sheria ya Usimamizi wa Mazingira inasimamiwa hasa ufanyaji wa Tathmini ya Athari kwa Mazingira, Hongereni sana,” amesema Dkt. Jafo
Aidha amesisitiza utunzaji wa vyanzo vya maji ya Mto Kilombero na Ruaha na kuzitaja faida za mradi huu wa kufua umeme wa Bwawa la Mwalimu Nyerere kuwa ni upatikanaji wa umeme wa uhakika, udhibiti wa mafuriko na uanzishwaji wa kilimo cha maji.
Waziri Jafo ametaja faida nyingine kuwa ni kupunguza matumizi ya nishati ya kuni na mkaa kwa ajili ya kupikia pamoja na kuongeza ujuzi kwa wataalamu nchini.
Ameongezeka kuwa kukamilika kwa mradi kutawezesha ongezeko la mapato kwa Serikali, upatikanaji wa maji, kuanzisha utalii wa maji kwa njia ya boti pamoja na kutunza ikolojia ya hifadhi ya Wanyama ya Selous.