Habari
Utekelezaji wa Bajeti 2026/27, Dira 2050 waanza
Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais inatarajia kuanza utekelezaji wa Bajeti ya mwaka wa fedha 2026/27 pamoja na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ambayo nguzo yake ya tatu inazungumzia Uhifadhi wa Mazingira na Ustahimilivu wa Mabadiliko ya Tabianchi, hatua inayokuja baada ya kuanzia kwa mwaka mpya wa fedha 2026/27 ulioanza leo Julai mosi.
Katika bajeti hiyo, Ofisi ya Makamu wa Rais iliidhinishiwa na Bunge bajeti ya shilingi bilioni 99.9 kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Ofisi zikiwemo za kudumisha Muungano, kusimamia Mazingira na Uchumi wa Buluu.
Katika hotuba aliyowasilisha Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni pamoja na kutoa ufafanuzi wa hoja za wabunge, alieleza mafanikio ya Ofisi hiyo katika kutatua hoja za Muungano.
Alisisitiza kuwa ni wakati muafaka wa kuzungumzia fursa za Muungano badala ya hoja za Muungano ambazo kimsingi Kamati ya Pamoja ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeendelea kuzipatia ufumbuzi.
Kwa upande wa Mazingira alilieleza Bunge kuhusu namna Ofisi ya Makamu wa Rais inavyoendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuhakikisha hifadhi ya mazingira inakuwa endelevu na kukukuza uchumi hususan kupitia biashara ya kaboni na uchumi wa buluu.
Aidha, Mkutano huo wa Bunge pia ulihusisha vipindi vya maswali na majibu ambayo yalijibiwa na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Reuben Kwagilwa kwa niaba ya Waziri wa Nchi.
Miongoni mwa masuala yaliyojitokeza ni pamoja na ufafanuzi kuhusu namna Serikali ilivyofanikiwa kudhibiti uzalishaji na uingizaji wa mifuko ya plastiki iliyopigwa marufuku kupungua kwa asilimia 95 hatua iliyochangia kupunguza uzalishaji wa taka za plastiki katika maeneo mbalimbali nchini.
Masuala mengine ni na Serikali utekelezaji wa mradi wa kuimarisha utayari wa Zanzibar kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi wenye thamani ya shilingi bilioni 1.3 zilizotoleewa na Mfuko wa Mabadiliko ya Tabianchi (GCF), zitatumika kutekeleza mradi huo ambao utaanza mara baada ya tathmini ya athari za mabadiliko ya tabianchi kukamilika.
Halikadhalika, Naibu Waziri Kwagilwa kupitia majibu ya serikali alielezea namna inavyohamasisha uwekezaji katika sekta ya usimamizi wa taka hususan taka ozo zinazozalishwa katika vyanzo mbalimbali kama hoteli, masokoni na majumbani masokoni na majumbani.



