Habari
Makamu wa Rais ateta na Katibu Mkuu OACPS
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi amekutana na kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Afrika, Karibiani na Pasifiki (OACPS) Mhe. Moussa Saleh Batraki, mazungumzo yaliyofanyika Jijini Arusha.
Katika Mazungumzo hayo, Makamu wa Rais amemuhakikishia Katibu Mkuu wa OACPS dhamira ya Tanzania kuendelea kutoa ushirikiano kwa Taasisi hiyo katika kuleta mageuzi na kuifanya kuwa na tija kwa nchi wanachama.
Aidha amempongeza Katibu Mkuu wa Jumuiya ya OACPS kwa kutekeleza ajenda ya mageuzi ikiwa ni pamoja na kuongeza uadilifu na kupunguza utegemezi kwa lengo la kufanya Taasisi hiyo kuwa na nguvu zaidi.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Afrika, Karibiani na Pasifiki (OACPS) Mhe. Moussa Saleh Batraki ameeleza kuhusu vipaumbele vya Taasisi hiyo ikiwemo suala la kuimarisha biashara, kuimarisha mtangamano miongoni mwa nchi wanachama, kujenga uhimilivu katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Pia ameeleza dhamira ya Taasisi hiyo ya kuweka kipaumbele na uwekezaji katika TEHAMA, hususani katika teknolojia za kidijitali, akili unde, ulinzi na usimamizi wa takwimu na taarifa. Pia kuimarisha mahusiano ya kibiashara miongoni mwa nchi zinazoendelea pamoja na kuwajengea uwezo wanawake katika masuala ya kiuchumi.
Mazungumzo hayo yamehudhuriwa na Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji na Umoja wa Ulaya Mhe. Jestas Nyamanga pamoja na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika Ellen Maduhu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.



