Habari
Dkt Muyungi akoshwa Kijiji cha Mazingira
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Richard Muyungi amevutiwa na Kijiji cha Mazingira katika Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya 50 (Sabasaba) yanayoendelea jijini Dar es Salaam.
Akizungumza wakati akitembelea maonesho hayo alisema kilichomvutia zaidi ni kuona namna ambavyo vijana wabunifu wamepewa nafasi ya kuonesha ujuzi wao katika kutumia fursa zinazopatikana kwenye Mazingira kupitia kampeni ya Taka ni Fursa.
Dkt. Muyungi alisisitiza umuhimu wa kuwawezesha vijana wenye mitaji midogo ili waweze kufanya mambo makubwa kupitia ubunifu wao kwenye kutumia fursa mbalimbali za urejelezaji na uchakataji taka ili kujipatia kipato na kusafisha Mazingira.
Aliambatana na Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Dkt. Immaculate Sware Semesi alipotembelea Kijiji cha Mazingira mara baada ya kushiriki hafla ya ufunguzi wa maonesho hayo Julai 3, 2026.



