Waziri Jafo atoa wito kwa wakurugenzi kutenga bajeti ya mazingira

Apr, 13 2023

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo ametoa wito kwa wakurugenzi wa halmashauri nchini kutoa kipaumbele kwa sekta ya mazingira kwa kutenga bajeti kwa ajili ya ununuzi wa miche ya miti.

Dkt. Jafo ametoa wito huo alipofanya ziara ya kikazi ya kukagua Mradi wa ujenzi wa josho la kuogeshea mifugo katika Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma leo Aprili 13, 2023.

Amesema kumekuwa na changamoto kwa maafisa mazingira katika wilaya nchini kutokuwa na bajeti ya kwa ajili ya shughuli za upandaji miti hali inayosababisha waonekane hawatekelezi majukumu yao ipasavyo.

Waziri Jafo amewataja maafisa hao wilayani kuwa wana kazi kubwa ya kuhakikisha maeneo yao yanapandwa miti ili kukabailiana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Amesema kipaumbele cha afisa mazingira ni mazingira yenyewe hivyo ni wakati sasa wa kila halmashauri kuwa na bajeti kwa maafisa hao ili kuwawezesha kutekeleza majukumu yao.

"Tunapomzungumzua Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan anavyotuongoza katika mapambano dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi maana yake anapambana kuhakikisha mazingira yanahifadhiwa, hivyo na afisa mazingira anatakiwa awe na nguvu hata siku ikitokea apande miti elfu tatu basi awe na bajeti.

“Tunatarajia afisa mazingira awe na kitalu cha halmashauri maalumu lakini kwa bahati mbaya maafisa mazingira hawawezishwi hata milioni tatu kwa mwaka," amesema Dkt. Jafo.

Aidha, waziri huyo amebainisha kuwa, bajeti hiyo ikitengwa kwa kila halmashauri itasaidia vijana waliokuwa katika halmashauri husika kupata shughuli za kufanya za kustawisha miche ambayo itanunuliwa na hivyo itasaidia kutengeneza ajira kwa vijana na hata urejeshaji wa mkopo wa asilimia 10 utakuwa rahisi.

Katika hatua nyingine Dkt. Jafo amewata wanachi kushirikiana na Serikali katika kutunza miradi ukiwemo Mradi wa Ujenzi wa Josho la kuogeshea mifugo.

Baadhi ya wananachi wameipongeza Serikali kwa kuwapelekea mradi huo na kusema utakuwa mkombozi kwao kama wafugaji kwani wafugaji utasaidia kuwaondolea adha ya kutembea umbali mrefu kufuata huduma hiyo.

Josho hilo limekamilika kwa asilimia 90 na shughuli za uogeshaji zinaendelea na kilichobaki ni kuchimba shimo ili iwe rahisi kubadilisha maji ya josho yaliyotumika.

Settings