Waziri Dkt. Jafo ashiriki Mkutano wa UNEA6 Kenya

Feb, 08 2024

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo anashiriki Mkutano wa Sita wa Baraza la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEA6) unaofanyika katika Makao Makuu ya Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) jijini Nairobi, Kenya.

Lengo kuu la mkutano huu ni kuandaa Sera kuhusu mazingira ambayo inalenga kurejesha maelewano kati ya binadamu na mazingira ili kuboresha maisha ya watu wanaokabiliwa na changamoto za mazingira

Mkutano wa UNEA6, unakutanisha viongozi kutoka mataifa mbalimbali duniani ikiwemo Tanzania kujadili masuala mbalimbali ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, uharibifu wa bioanuai na uchafuzi wa mazingira.

Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazokabiliwa na athari za mabadiliko ya tabianchi ambayo husababisha ukame, uhaba wa mvua, mafuriko na vifo vya mifugo.

Hivyo, katika kukabiliana na changamoto hizo Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za kukabiliana na athari hizo.

Aidha, mkutano huu unatoa fursa kwa Serikali za nchi 193 wanachama wa Umoja wa Mataifa, wanaharakati wa mazingira, wanasayansi, sekta binafsi , taasisi za fedha na asasi za kiraia kupaza sauti na kuhusishwa katika kutunga sera ya ulimwengu mzima kuhusu mazingira.

Kaulimbiu ya Mkutano wa UNEA6 kwa mwaka 2024 ni 'Juhudi Madhubuti, Jumuishi na Endelevu za Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi, Uharibifu wa Bioanuai na Uchafuzi‘.

Aidha, Ujumbe wa Tanzania ulioambatana na Waziri Dkt. Jafo ni Naibu Katibu Mkuu (Muungano) Ofisi ya Makamu wa Rais Bw. Abdallah Hassan Mitawi na wataalamu kutoka Ofisi hiyo.

Mkutano wa UNEA6 ulifunguliwa Februari 26, 2024 na unatarajiwa kuhitimishwa Machi 01, 2024.

Settings