Habari
Watumishi Ofisi ya Makamu wa Rais wahimizwa mshikamano
Watumishi wa Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) wamehimizwa kuendelea kuishi kwa Umoja, Upendo na mshikamano ili kuenzi misingi ya mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Rai hiyo imetolewa Machi 18, 2026 Jijini Dodoma na Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo, Dkt. Richard Muyungi wakati wa hafla ya iftar aliyoiandaa kwa watumishi wa Ofisi huku akiwakumbusha umuhimu wa kuzingatia misingi ya toba ya mwezi huo.
Dkt. Muyungi ameeleza kuwa iftar imeandaliwa kwa dhamira mahsusi hiyo mahsusi ya kushirikisha watumishi wote katika toba ya mwezi wa ramadhani na hivyo kuwaunganisha katika kutekeleza toba ya mwezi mtukufu na kipindi cha kwaresma.
“Tumeona ni jambo jema tukutane jioni kwa iftar hii ili tukimaliza mwezi wa ramadhani tuwe tumeshiriki kwa pamoja na hili ndio dhumuni letu kubwa la kukutana hapa kwani hii ni nguzo muhimu huku tukikumbushwa kuwa na umoja, upendo na mshikamano ndani ya ofisi yetu” amesema Dkt. Muyungi.
Aidha Dkt. Muyungi ameeleza kuwa suala la umoja, upendo na mshikamao liwe ni la kudumu ndani ya ofisi hiyo hata baada ya mwezi mtukufu wa ramadhani kukamilika kwani na jambo jema lililojenga na kuimarisha ufanisi na utendaji kazi.
Amesema katika kutekeleza kwa vitendo dhamira hiyo, Ofisi hiyo imeanzisha utaratibu wa kufanya mazoezi ya pamoja kwa watumishi wote hali inayojenga umoja, upendo na mshikamano baina yao..
Ameeleza kuwa misingi ya umoja, upendo na mshikamano ni nguzo muhimu katika kipindi hiki cha mwezi wa ramadhani kwa kuhakikisha watumishi wote wanakaa pamoja na kushirikishana katika masuala mbalimbali yanayowajenga katika imani na toba.
“Kukaa pamoja iwe asili yetu na tuendelee kushirikishana katika masuala mbalimbali ili tuwe ofisi moja na kuweze kufanya kazi kwa ufanisi na tukimaliza mfungo wa ramadhani tuendelee kuwa wamoja zaidi” amesema Dkt. Muyungi.



