Habari
Dkt Muyungi, Santiago Network wateta
Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Richard Muyungi amekutana na Mwakilishi wa Sekretarieti ya Santiago Network, Bw. Lorenzo Guadagno kwa lengo la kuimarisha ushirikiano kati ya Ofisi ya Makamu wa Rais na Santiago Network, pamoja na kujadili namna ya kuhakikisha kuwa Ofisi ya Kanda ya Santiago Network kwa Afrika iliyopo Dar es Salaam.
Kikao hicho kimefanyika pembezoni mwa Mkutano wa 64 wa Wataalam wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (SB64) unaofanyika Bonn, Ujerumani
Tanzania, inatekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kufikia malengo yaliyokusudiwakatika kusaidia nchi za Afrika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, hususan Hasara na Uharibifu (Loss and Damage).
Dkt. Muyungi alisisitiza dhamira ya Serikali ya Tanzania ya kuendelea kushirikiana na Santiago Network ili kuhakikisha kuwa ofisi hiyo ya kikanda inakuwa kitovu muhimu cha uratibu, ujenzi wa uwezo, kubadilishana uzoefu na utoaji wa msaada wa kiufundi kwa nchi za Afrika. Alieleza kuwa Tanzania iko tayari kutoa ushirikiano unaohitajika ili kuwezesha utekelezaji wa majukumu ya ofisi hiyo kwa manufaa ya bara la Afrika.
Kwa upande wake, Bw. Guadagno alieleza dhamira ya Sekretarieti ya Santiago Network ya kuimarisha ushirikiano na Tanzania na wadau wengine wa kikanda ili kuhakikisha kuwa huduma na msaada wa kiufundi unaotolewa kupitia ofisi ya Dar es Salaam unawafikia walengwa kwa wakati na kwa ufanisi, sambamba na malengo ya Santiago Network ya kusaidia nchi zinazoendelea kukabiliana na changamoto za hasara na uharibifu unaotokana na mabadiliko ya tabianchi.
Pande zote mbili zilikubaliana kuendelea kuimarisha mawasiliano na ushirikiano wa karibu ili kuhakikisha kuwa Ofisi ya Kanda ya Santiago Network kwa Afrika inakuwa chombo madhubuti cha kusaidia nchi za bara hilo katika kujenga ustahimilivu na kuimarisha uwezo wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.



