Habari
Makamu wa Rais awamwagia sifa waandishi waendesha ofisi
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi amesema Serikali inatambua umuhimu mkubwa wa Waandishi Waendesha Ofisi kwa kuwa ni muhimili muhimu katika kuwawezesha Viongozi na watendaji kutekeleza majukumu yao.
Makamu wa Rais amesema hayo, wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa 13 wa Kitaaluma wa Waandishi wa Waendesha Ofisi Tanzania (TAPSEA) unaofanyika katika Ukumbi wa Ngurdoto Mkoani Arusha. Amesema Serikali inaipa uzito Taasisi ya TAPSEA kwa kuwa inatambua ili kuwa na utulivu na mshikamano ni lazima Waandishi Waendesha ofisi kutimiza wajibu ipasavyo.
Amewapongeza Waandishi Waendesha Ofisi kwa kubeba sura za Taasisi wanazofanyia kazi kwa kuwa wakarimu na wenye kutoa msaada wa awali kwa wananchi wanaofika kutafuta huduma. Amewasihi kuendelea kutoa huduma kwa ukamilifu pamoja na kuwa na heshima na ukarimu ili kuwafariji wanaowahudumia.
Aidha Makamu wa Rais, amewasisitiza waandishi waendesha ofisi kuendelea kujitambua na kutunza siri wakati wa utekelezaji wa majukumu yao.
Makamu wa Rais amekipongeza Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania kwa kuimarisha elimu yao mpaka kufikia shahada ya uzamili ambayo imewawezesha Waandishi Waendesha Ofisi kuhama katika mfumo asili wa utekelezaji wa majukumu yao mpaka kufikia kuwa sehemu ya maamuzi ya kisera na upangaji wa mikakati na utekelezaji wake.
Amesisitiza kwamba Vyuo vinavyotoa mafunzo hayo, vinapaswa kuendelea kujiimarisha ili kuwa na waandishi waendesha ofisi wanaoweza kusaidia vema Taifa. Makamu wa Rais ametoa wito kwa Taasisi mbalimbali kuhakikisha wanawawezesha Waandishi Waendesha Ofisi kushiriki mikutano ya kitaaluma.
Halikadhalika, Makamu wa Rais amewapongeza Viongozi wa Taasisi hiyo wanaomaliza muda wao kwa kufanya kazi nzuri iliyowaunganisha na kuwawezesha Waandishi Waendesha Ofisi nchini. Aidha amewataka kufanya uchaguzi wa haki ili kupata Viongozi sahihi wanataoiongoza vema Taasisi hiyo. Amewasihi kufanya uchaguzi kwa kuzingatia uhuru na haki ili kupata viongozi sahihi wa Taasisi hiyo pamoja na kuwataka wanachama kuchagua viongozi makini bila ubaguzi wa aina yeyote.
Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Ridhiwani Kikwete, amesema Serikali kupitia ofisi hiyo, itaendelea kutoa ushirikiano kwa watumishi wote wa Umma ikiwemo uongozi wa TAPSEA ili kufanikisha masuala mbalimbali ya kiutumishi kwa wanachama wake.
Ameongeza kwamba, Ofisi hiyo itaendelea kuwaangalia na kuwalea wanaTAPSEA na kuwataka kuwa na imani na serikali inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa wataendelea kuwaangalia katika hali zote kiwemo maslahi yao, kutoa mafunzo pamoja na kuwahakikisha kuwa salama muda wote.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Waandishi Waendesha Ofisi Tanzania (TAPSEA) Bi. Zuhura Maganga amesema Taasisi hiyo inajivunia mafanikio yaliyopatikana katika kuimarisha taaluma ya uandishi uendesha ofisi ikiwemo kuanzishwa kwa shahada ya utawala inayotolewa na Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania pamoja kuanzishwa kwa shahada ya uzamili ya Sanaa katika mawasiliano na usimamizi wa ofisi.



