Habari
Serikali yafungua milango kwa wawekezaji fursa za mazingira
Serikali imetoa wito kwa wadau kutoka sekta mbalimbali ndani na nje ya nchi kushiriki kikamilifu katika mikakati ya urejelezaji wa taka ozo ili kulinda mazingira.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Reuben Kwagilwa ametoa wito huo alipokutana na ujumbe kutoka Kampuni inayojihusisha na urejelezaji wa taka taka ozo ya Biotech 22 Ltd kutoka Bulgaria, kwenye ukumbi wa Ofisi ya Makamu wa Rais jijini Dodoma leo Juni 10, 2026.
Wawekezaji hao waliwasilisha mapendekezo ya mradi wa Mradi wa kutumia teknolojia ya kubadilisha taka ozo kuwa malighafi ya kuzalilisha mboleo pamoja na kulinda mazingira yasiharibiwe.
Katika mazungumzo hayo, Mhe. Kwagilwa alisema kuwa wadau ni watu muhimu katika sekta ya usimamizi wa taka hususan taka ozo ambayo inawezesha usafi wa mazingira katika miji kwa kutoacha taka hizo kuzagaa ovyo.
Aliwapongeza wadau hao kwa kuja na mradi huo ambao utasaidia katika kulinda mazingira na kuwataka kushirikiana na taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Makamu wa Rais zikiwemo Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Kituo cha Taifa cha Kuratibu Kaboni (NCMC) pamoja na Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA ili kupata mwongozo wa uwekezaji.
Kwa upande wake Teodora Tomova kutoka Kampuni ya Biotech aliwasilisha pendekezo la Mradi wa kutumia teknolojia ya kubadilisha taka ozo kuwa malighafi ambayo hutumika kudhibiti mmomonyoko wa ardhi na kurejesha maeneo yaliyoharibiwa na shughuli za uchimbaji.
Alitaja faida zingine kuwa ni pamoja na kuboresha rutuba ya udongo kupunguza uchafuzi wa maji na mazingira, kupunguza methane na hewa ukaa sanjari na kutumia fursa ya biashara ya kaboni.
Aidha, Tomova alisema kuwa mapendekezo ya mradi huo ni kuanza na majaribio ya utekelezaji kwa kipindi cha mradi miezi 12 mkoani Dar es Salaam ili kuonesha uwezo wa teknolojia hii katika kulinda mazingira ya pwani.
Kikao hicho kimehudhuriwa na Naibu Katibu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais Balozi Baraka Luvanda, Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Mazingira Dkt. Paul Deogratius, Ujumbe kutoka Data Vision International wanaosimamia miradi na wataalamu kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais.



