Ujenzi wa ukuta wa bahari Nungwi Zanzibar wanukia

Nov, 06 2023

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis amesema Serikali inatarajia kuanza tathmini ya ujenzi wa ukuta katika fukwe za Bahari ya Hindi maeneo ya Nungwi Mkoa wa Kaskazini, Zanzibar.

Amesema kwa kuwa fedha zimeshapatikana, andiko limewasilishwa kwa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kwa ajili ya michoro kuainisha aina ya ukuta unaotakiwa kujengwa.

Mhe. Khamis amesema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Nungwi Mhe. Simai Hassan Sadiki aliyetaka kujua ni lini tathmni ya ujenzi wa ukuta katika maeneo yaliyoathiriwa na bahari Nungwi.

Naibu Waziri amefafanua kuwa kabla ya kujenga ukuta Serikali itafanya utafiti kujua ni aina gani ya ukuta unaofaa kujengwa katika eneo hilo ambao utasaidia kuzuia mawimbi yasifike kwenye makazi ya wananchi ili waendelee kufanya shughuli za kiuchumi.

Amesema Serikali imechukua hatua mbalimbali za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi katika maeneo mbalimbali ya fukwe za Bahari ya Hindi.

“Kwa mwaka wa fedha 2023/24 Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar imetenga fedha jumla ya shilingi milioni 650 kwa ajili ya tathmini ya awali ili kufanya usanifu wa miundombinu itakayosaidia kurudisha fukwe katika hali yake,” amesema Mhe. Khams.

Ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, amewahimiza wananchi wa maeneo ya Nungwi kuongeza jitihada za kupanda mikoko ambao inasaidia kupunguza mawimbi ya bahari katika fukwe pamoja na kutochimba mchanga kiholela.

Pia, Naibu Waziri Khamis amewataka wananchi kuacha kutupa taka ovyo katika fukwe ili kulinda mazingira huku akiwapa rai kuhamasisha ulimaji na uvunaji wa mwani usioharibu fukwe.

“Napenda kuchukua nafasi kuhimiza uongozi na wananchi wa Nungwi kuongeza jitihada za kutunza mazingira ya maeneo ya ufukwe wa Nungwi kwa kudhibiti shughuli zisizo endelevu za kibinadamu kwa kuingeza jitihada za kuhifadhi mazingia na upandaji wa miti” amesisitiza.

Kwa upande mwingine amesema ili kutatua changamoto ya shughuli za uvuvi usiozingatia hifadhi ya mazingira na matumizi ya fukwe yasiyo endelevu, Serikali imechukua hatua mbalimbali zikiwemo kutoa elimu kwa wavuvi na wananchi kwa ujumla wajikite katika uvuvi rafiki kwa mazingira.

Hali kadhalika Mhe. Khamis amesema kuwa Serikali kwa kushirikiana na vyombo mbalimbali inafanya doria katika maeneo ya bahari na kuchukua hatua za kuangamiza nyavu zinazotumika katika uvuvi haramu kwa lengo la kuhifadhi mazingira ya bahari.

Settings