Habari
Tanzania yaendelea kufungua fursa biashara ya kaboni
Serikali ya Tanzania imeingia makubaliano na kampuni mbili kutoka Japan kwa ajili ya kufungua fursa za soko la biashara ya kaboni kupitia mpango wa Uratibu wa Pamoja wa Mikopo (JCM), hatua inayolenga kuongeza mchango wa sekta binafsi katika kufanikisha dira ya taifa ya maendeleo ya mwaka 2050.
Akizungumza katika warsha ya kusaini Hati ya makubaliano hayo, Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Richard Mayungi, alisema serikali ina jukumu la kuhakikisha dira ya 2050 inafikiwa kupitia uwekezaji katika nishati safi, biashara ya kaboni na udhibiti wa taka.
Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa Kituo cha Biashara ya Kaboni (NCMC), Kathryn Kigaraba, alibainisha kuwa utoaji wa mikopo kwa pamoja utasaidia kulinda mazingira, kukuza biashara na kuongeza mapato ya Serikali.
Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa kampuni ya 3T kutoka Japan, Kan Shimizu, alisema Tanzania itanufaika kwa kiasi kikubwa kupitia ushirikiano huu, hususani katika sekta ya utunzaji wa mazingira na biashara ya kaboni
Makubaliano haya ya ushirikiano kati ya NCMC na kampuni za Japan yanalenga kuchochea mchango wa sekta binafsi katika kufanikisha malengo ya Dira ya taifa ya mwaka 2050, ambapo nguzo ya tatu ya Dira hiyo inasisitiza ukuaji wa uchumi wa Taifa na maendeleo endelevu yanayozingatia mazingira endelevu.



