Serikali yaendelea kutatua hoja za Muungano zilizosalia

Jan, 19 2024

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Khamis Hamza Khamis amesema tangu kuanzishwa kwa utaratibu wa kushughulikia hoja za Muungano kupitia vikao vya Kamati ya Pamoja ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SJMT) na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) hoja 22 kati ya 25 za Muungano zimepatiwa ufumbuzi.

Mhe. Hamza amesema hayo alipokuwa akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa maadhimio ya Bunge yatokanayo na taarifa ya kamati ya kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria katika kikao kilichofanyika Dodoma Januari 19, 2024.

Amesema Ofisi inafanya ufuatiliaji wa utekelezaji wa maagizo na maamuzi ya Kamati ya Pamoja ya SJMT na SMZ ya kushughulikia masuala ya Muungano na kufanya ziara za ufuatiliaji wa utekelezaji wa majukumu ya taasisi za Muungano kwa pande zote mbili.

“Ofisi imeendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu na faida za Muungano ikiwemo hatua zilizochukuliwa kutatua hoja za Muungano. Elimu hiyo imetolewa kupia machapisho mbalimbali, vyombo vya habari, makongamano, maonyesho ya shughuli mbalimbali za kitaifa, majarida na vipeperushi.

“Serikali imekuwa ikifanyia kazi makubaliano ambayo yamefikiwa katika utatuzi wa hoja kwa kufanya ziara za ufuatiliaji wa utekelezaji wa majukumu ya Taasisi za Muungano kwa pande zote mbili za Muungano,” amesema Mhe. Khamis.

Ameongeza kwamba Serikali imekuwa ikifanya jitihada za makusudi kuhakikisha elimu kwa umma inatolewa ikiwa pamoja na kuandaa na kusambaza kitabu cha historia ya Muungano kupitia vyombo vya habari, machapisho na makongamano.

“Tumekuwa tukiandaa na kusambaza majarida ya hoja zilizopatiwa fumbuzi na hatua mbalimbali zilizochukuliwa, kupitia maadhimisho ya Muungano (2023), Maonyesho ya Taasisi za Muungano yaliyofanyika Zanzibar (2022), Maonyesho ya Nanenane (2023) mkoani Mbeya, Vikao vya Kamati ya Pamoja kati ya SJMT na SMZ Pamoja na Hotuba za viongozi wa Ofisi ya Makamu wa Rais.

Ofisi ya Makamu wa Rais ina jukumu la kuratibu masuala ya Muungano na kuimarisha ushirikiano katika masuala yasiyo ya Muungano.

Settings