Serikali yaelekeza wataalamu wa mazingira kushughulikia magugu maji Ziwa Jipe

Sep, 20 2021

Serikali imeelekeza wataalamu wa mazingira kufika katika Ziwa Jipe wilayani Mwanga Mkoa wa Kilimanjaro na kufanya upembuzi yakinifu utakaosaidia kuyaondoa magugu maji yaliyozingira ziwa hilo.

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Hamad Hassan Chande Chande ametoa maelekezo hayo Septemba 20, 2021 alipofanya ziara ya kikazi kukagua athari za kuenea kwa magugu maji hayo.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo alitahadharisha kuwa kutoweka kwa ziwa hilo kunaweza kusababisha madhara makubwa kwa Taifa kwani wananchi wanaweza wakapoteza fursa za uwekezaji.

“Nimejionea madhara ya magugu maji katika ziwa hili jambo ambalo linaweza kusababisha likapotea kabisa katika ramani hivyo naelekeza wataalamu wetu wa mazingira wajiridhishe kabla ya kuomba fedha kutoka kwa wahisani wa ndani na nje watusaidie fedha ili kuondoa magugu haya,” alisema.

Kutokana na changamoto ya kutofanyika kilimo endelevu, Chande aliutaka Uongozi wa Wilaya ya Mwanga pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama kuhakikisha wanadhibiti kilimo kisicho endelevu kando ya ziwa ambacho husababisha athari za kimazingira ikiwemo mmomonyoko wa udongo.

Katika kuhakikisha mipaka ya ziwa hilo inalindwa aliwahakikishia wananchi kuwa suala hilo litafanyiwa kazi kwa kuhusisha nchi zote mbili yaani Tanzania na Kenya ili Watanzania wafaidi rasilimali zao.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Mwanga, Mhe. Joseph Tadayo aliiomba Serikali kutatua changamoto hiyo kwa kuondoa magugu hayo ndani ya ziwa akisema kuwa linategemewa kwa shughuli mbalimbali zikiwemo uvuvi, mradi mkubwa wa maji wa Same, Mwanga na Korogwe pamoja na kilimo cha umwagiliaji.

Tadayo alisema ziwa hilo litasaidia kuongeza ajira hususan kwa vijana na hivyo kunufaisha wakazi zaidi ya 2,000 wanaolizunguka pamoja na baadhi ya wananchi wa Wilaya jirani ya Moshi Vijijini.

Kwa upande wake Meneja wa Kanda ya Kaskazini wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Bw. Lewis Nzali alisema kuna mradi umendaliwa kwa ajili ya kulinusuru Ziwa Jipe na hatua ya kutafuta wafadhili imeanza.

“Kwenye Kanda yetu kuna miradi mitatu ambayo ni Ziwa Babati na kule Hanang Ziwa Basoutu ambako kuna changamoto ya kujaa maji na tulikwenda kule mwa mwaka jana tulikuta baadhi ya nyumba zimezingirwa kwa maji. Ziara hii itahuisha kufuatilia kwa karibu miradi hii,” alisema Nzali.


Awali akisoma taarifa, Afisa Mazingira wa Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga, Bw. Elirehema Palanjo alisema ziwa hilo linakabiliwa n\a changamoto ya usimamizi wa kimazingira.

Alisema kuwa Wilaya itahamsisha jamii kusimamia vyanzo vya maji, kuhifadhi mazingira na mbinu za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kudhibiti shughuli zinazoweza kusababisha uharibifu wa mazingira.

Settings