Serikali yaandaa mpango wa kukabili mabadiliko ya tabianchi kwenye fukwe

May, 22 2023

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis amesema Serikali imeandaa mpango kabambe wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi katika fukwe za Bahari ya Hindi.

Amesema hayo leo Mei 22, 2023 wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu Mhe. Amina Daudi Hassan aliyetaka kufahamu mpango wa Serikali kutenga fedha za mabadiliko ya tabianchi kusaidia wananchi wenye visima vya maji chumvi Zanzibar.

Naibu Waziri Khamis alisema kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SJMT) ikishirikiana na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) inatekeleza miradi mbalimbali ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa pande mbili za Muungano ambayo inahusika na uchimbaji wa visima.

Alifafanua kuwa kwa upande wa Zanzibar, Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa kutumia Mifumo Ikolojia Vijijini (EBBAR) umechimba visima sita katika Wilaya ya Kaskazini ‘A‘.

Aliongeza kuwa Mradi wa Kurejesha Ardhi iliyoharibika na Kuongeza Usalama wa Chakula (LDFS) umechimba visima viwili katika Shehia ya Maziwa Ng’ombe na Shehia ya Kiuyu Mbuyuni katika Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini, Pemba.

“Katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi katika maeneo ya fukwe za Jambiani, Paje na Nungwi, Serikali imekuwa ikiwaelimisha wananchi kupanda mikoko, kuacha kutupa taka katika fukwe, kutofanya uchimbaji holela wa mchanga, lakini pia ulimaji na uvunaji wa mwani usiharibu fukwe," alisisitiza.

Hata hivyo, Mhe. Khamis aliongeza kuwa Serikali imeanza kutekeleza mradi wa ujenzi wa kuta za bahari ukiwemo wa Mikindani mkoani Mtwara na Sipwese Mkoa wa Kusini, Pemba ili kupunguza kasi maji chumvi kutoka baharini kuingia kwenye makazi ya wananchi.

Katika hatua nyingine alisema Serikali itafanya tafiti katika maeneo mengine ya visiwa vya Zanzibar yakiwemo fukwe ili kuona ni aina ya gani ya ukuta ambao unafaa kujengwa ili kuwasaidia wananchi kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Settings