Habari
Ofisi ya Makamu wa Rais na Benki ya NBC wajadili ushirikiano
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Richard Muyungi amekutana na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Mikakati wa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) Bw. Msafiri Shayo yaliyolenga kujadili ushirikiano.
Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika Mei 26, 2026 Jijini Dar es Salaam, Dkt. Muyungi ameipongeza benki hiyo kongwe nchini kwa kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali za uhifadhi na usimamizi wa mazingira nchini na mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.
Dkt. Muyungi amesema Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais itaendelea kushirikiana kwa karibu na benki hiyo katika kuhakikisha inakamilisha mchakato wa kupata ithibati kutoka mfuko wa dunia wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi (GCF).
“Upatikanaji wa ithibati hiyo utasaidia nchi kuzifikia fedha za mabadiliko ya tabianchi na hivyo kuwezesha kufikia malengo ya Dira 2050 kupitia nguzo ya tatu inayohusu masuala ya uhifadhi wa mazingira na ustahimilivu wa mabadiliko ya tabianchi” amesema Dkt. Muyungi.
Aidha ameeleza kuridhishwa na dhamira ya benki hiyo ya kuendeleza mashirikiano na Serikali katika kutekeleza mipango ya muda mfupi, kati na mrefu inayohusu masuala ya mazingira ikiwemo Programu ya Mageuzi ya Kimkakati ya Mazingira Endelevu Tanzania (2026-2030).
Dkt. Muyungi ameiomba Benki hiyo kuendeleza masuala ya ujuzi kwa wataalamu wakati wa kuandaa ripoti kupitia mfumo jumuishi wa mazingira, kijamii na utawala (ESG) katika sekta zote nchini.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mikakati wa Benki ya NBC, Bw. Msafiri Shayo amesema Benki hiyo imekuwa na mashirikiano ya muda mrefu na Ofisi ya Makamu wa Rais katika utekelezaji wa kampeni na programu mbalimbali za masuala ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi.
Aidha Bw. Shayo ameiomba Serikali kufanikisha mchakato wa benki hiyo kupata ithibati kutoka Mfuko wa dunia wa mabadiliko ya tabianchi (GCF) kwani fedha hizo zitasaidia utekelezaji miradi mbalimbali ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi.
Kikao hicho kilihudhuriwa pia na watendaji waandamizi kutoka Benki ya NBC akiwemo Mkuu wa Biashara ya Serikali, Bi. Joyce Maruba na Meneja Mahusiano Taasisi za Serikali, Bw. Azza Mnzava na maofisa kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais.



