Naibu Waziri Khamis ahamasisha matumizi ya nishati mbadala kupunguza ukataji miti

Feb, 26 2023

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis ametoa rai kwa wizara na taasisi katika sekta za umma na binafsi kutumia nishati mbadala ili kupunguza ukataji wa miti kwa ajili ya matumizi ya kuni na mkaa

Mhe. Khamis amesema hayo Februari 25, 2023 wakati wa uzinduzi wa kampeni ya ‘Soma na Mti’ katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino jijini Mwanza ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha upandaji miti na utunzaji wa mazingira katika taasisi za elimu ya juu nchini.

Amesema zoezi la upandaji katika maeneo mbalimbali nchini ni ajenda ya kitaifa inayoongozwa na viongozi wa kitaifa akiwemo Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais Mhe.Dkt Philip Mpango na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa na hivyo kuzitaka taasisi za umma na binafsi kuunga mkono juhudi hizo.

“Tupo hapa kutekeleza mpango wa Serikali juu ya utunzaji wa mazingira ikiwa ni muendelezo wa juhudi zilizoanzishwa na viongozi wetu wakuu wa kitaifa. Nitoe rai kwa viongozi wa ngazi zote kuhakikisha tunasimamia maelekezo ya Serikali ya kuzuia ukataji miti, tuanze kutumia nishati mbadala kama gesi kwa ajili ya kupikia kama anavyosisitiza Rais wetu,” amesema Mhe. Khamis

Aidha naibu waziri huyo ametoa maagizo kwa wakurugenzi wa halmashauri zote nchini kuhakikisha kuwa wanasimamia na kuendeleza kampeni hiyo kwa kuhakikisha kila shule na kila mwanafunzi anakuwa na mti wake na kuhimiza utamaduni wa kila Kaya kupanda miti na kila mtu anayenunua eneo kuhakikisha amepanda miti katika eneo lake.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Mhe. Amina Makilagi amesema suala mazingira ni moja ya kipaumbele vya msingi kinachotekelezwa na taasisi zote za umma na binafsi zilizopo katika Wilaya hiyo na kukusudia kulifanya Jiji la Mwanza kuendelea kuwa Jiji la kijani.

“Katika Wilaya ya Nyamagana kila mradi unaotekelezwa unafungamanishwa na mazingira na kila tukio tunapanda miti na hivi karibuni taasisi zetu za TFS, Gereza la Butimba na wadau wengine tulipanda zaidi ya miti 7000 katika vyanzo mbalimbali vya maji ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Mhe. Makamu wa Rais,” amesisitiza Makilagi.

Ameongeza kuwa kupitia kampeni ya “Soma na Mti” wilaya hiyo imejipanga kimkakati katika kuhakikisha kuwa inafikia lengo la kupanda miti 1,500,000 kwa kushirikisha shule za msingi, sekondari na taasisi za elimu ya juu na kuhakikisha inarejesha hadhi ya Jiji la Mwanza kuwa kinara wa usafi wa mazingira nchini.

Naye Balozi wa Mazingira Nestory Mushi amesema kupitia taasisi yake ya Mweka Site wamefanikiwa kuotesha miti zaidi ya 358,000 na miti hiyo inatarajia kupandwa katika Mikoa yote inayokabiliwa na hali ya ukame.

Taasisi yetu inahamisha jamii katika shughuli zote za usafi wa mazingira ikiwemo upandaji miti na usafi wa fukwe mbalimbali. Tunafundisha wanafunzi wa ngazi mbalimbali ikiwemo shule za msingi, sekondari na vyuo vikuu kuhusu vitalu vya miti, miradi ya samaki na utunzaji mazingira” amesema Mushi.

Mwakilishi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Alex Julius amesema katika kuunga mkono juhudi za Serikali kuhamasisha utunzaji wa mazingira ikiwemo upandaji, TFS imeanzisha kitalu cha miti ya matunda na vivuli ambapo kati ya Julai 2022 hadi Februari 2023, TFS imefanikiwa kuzalisha miche ya miti 67,310.

Wakati wa kuzalisha miche hii tunazingatia masuala mbalimbali ikiwemo miche inayokuwa haraka, miche inayohifandhi maji, miche inayozuia mmomonyoko wa udongo na kuanzia mwezi Julai 2022 hadi Februari 2023 miche ya miti 32,970 imegawiwa bure katika taasisi mbalimbali” amesema Julius.

Kampeni ya “Soma na Mti” ilizindiliwa na Ofisi ya Makamu wa Rais mwaka 2022 ikiwa imelenga kuhamasisha wanafunzi wa shule za msingi, sekondari na vyuo vikuu kuona zoezi la upandaji miti kuwa sehemu muhimu ya maisha ili kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.

Settings