Kiongozi wa Mbio za Mwenge aonya uharibifu wa vyanzo vyanzo vya maji

May, 25 2023

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2023 Abdalla Shaibu Kaim amewataka wananchi kuacha kufanya shughuli za kibinadamu zikiwemo kilimo na ufugaji karibu na vyanzo vya maji.

Ametoa kauli hiyo leo Mei 25, 2023 wakati wa mbio za Mwenge wa Uhuru kukagua mradi wa utunzaji mazingira unaotekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) Manispaa ya Kigamboni mkoan Dar es Salaam.

Shaib amesisitiza kuwa hairuhusiwi kwa mtu yeyote kufanya shughuli hizo ndani ya mita 60 kutoka kwenye vyanzo vya maji kwani ni kinyume cha sheria na ni uharibifu wa Mazingira.

Alisema ni muhimu kulinda na kuviendeleza vyanzo vya maji pamoja na uoto wa asili ikizingatiwa kuwa maji ni uhai hatua inayoenda sambamba na kuunga mkono juhudi za Serikali za upandaji miti kwenye vyanzo vyetu vya maji na kuitunza.

Aidha, Kiongozi huyo alitumia nafasi hiyo kuipongeza DAWASA kwa jitihada kubwa wanazofanya za kulinda na kuendeleza mazingira kwa kutunza vyanzo vya maji.

Kwa upande wake Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Kiula Kingu alisema katika jitihada za kutunza na kuendelea vyanzo vya maji katika mradi wa maji Kigamboni, Mamlaka imefanikisha kupanda miti ya matunda na kivuli takribani miti 3,300.

Mbio za Mwenge wa Uhuru zinaendelea katika mikoa mbalimbali na kwa mwaka 2023 unachagizwa na kaulimbiu isemayo “Tunza Mazingira, Okoa vyanzo vya Maji kwa Ustawi wa Viumbe hai na Uchumi wa Taifa”.

Settings