Mkutano wa COP 28 wailetea neema Tanzania

Dec, 18 2023

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo amesema Tanzania inatatarajia kunufaika na fedha za miradi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi huku kampuni 56 zikionesha nia ya kuwekeza nchini.

Ametoa kauli hiyo Desemba 18, 2023 jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ushiriki wa Tanzania katika Mkutano wa 28 wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP 28) uliofanyika Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu.

Dkt. Jafo amesema kupitia mikutano ya pembezoni iliyohusisha majadiliano kati ya Tanzania na wadau kutoka nchi, uliofanyika Novemba 30 hadi Desemba 12, 2023 Tanzania itanufaika na teknolojia na Programu ya Afrika ya Nishati Safi ya Kupikia pamoja na afya.

Amesema kuwa programu hiyo inaunga mkono juhudi za Serikali za kuhamasisha kuachana na matumizi ya kuni na mkaa ambayo yanasababishwa na ukataji wa miti.

Pamoja na manufaa hayo, Waziri Jafo amesema kuwa pia utekelezaji wa mikakati ya kuimarisha uhimili katika katika sekta ya maji, misitu na bahari ambayo ni mojawapo ya rasilimali muhimu kwa uchumi wa buluu.

”Mkutano huo umekuwa na mafanikio kwani tumejadili fursa za uwekezaji kwenye sekta ya kilimo katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi hivyo kuongeza kasi ya kupambana na mabadiliko ya tabianchi.

“Tumejadili mikakati ya kukusanya Dola za Marekani bilioni 1.8 kwa ajili ya kuchimba visima 65,000 ambapo kila kisima kimoja kitahudumia wakulima wenye mashamba ya ukubwa wa hekta 2.5 huku wadau wa maendeleo waliahidi kuchangia programu hii Dola za Marekani milioni 610,” amesema huku akiongeza kuwa programu hiyo itasaidia uhimilivu wa mabadiliko ya tabianchi katika sekta ya Kilimo na itapunguza uharibifu wa mazingira.

Halikadhalika amebainisha kuwa katika kuwezesha ushiriki kikamilifu, Tanzania iliandaa msimamo wa taifa uliosaidia kuongoza dira ya ushirikiri na majadiliano ya wajumbe wa Tanzania, ulioandaliwa kwa ushirikianao na wadau mbalimbali.

Aidha, Dkt. Jafo amebainisha kuwa kaulimbiu wa Tanzania ilikuwa ni ‘Kuimarisha Hatua za Kilimo Himilivu na Uchumi wa Bluu’, iliyolenga kuchochea hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa kuwa na kilimo endelevu na kutumia vizuri fursa za uchumi wa buluu.

Hivyo, Mkutano wa 29 (COP 29) umepangwa kufanyika nchini Azerbaijan kuanzia Novemba 11 hadi 22, wakati COP30 itafanyika nchini Brazil kuanzia Novemba 10 hadi 21, 2025.

Settings