Mitawi: Vyombo vya Habari ni wadau muhimu wa Elimu ya Mazingira

Sep, 17 2023

Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais imesema itaendelea kushirikiana na vyombo vya habari nchini katika kutoa wa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa uhifadhi na utunzaji wa mazingira ikiwemo wa uhifadhi wa Tabaka la Ozoni.

Hayo yamesemwa na Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Bw. Abdallah Mitawi wakati akifungua warsha ya mafunzo kwa waandishi wa vyombo vya habari kuhusu udhibiti wa uingizaji wa kemikali zinazodhibitiwa chini ya Itifaki ya Montreal iliyofanyika Septemba 16, 2023 jijini Dar es Salaam.

Mitawi amesema Tanzania kama nchi nyingine Duniani imeendelea kuwa mstari wa mbele katika kukabiliana athari za matumizi vifaa vya kemikali vyenye ukomo wa matumizi kwa kuimarisha mifumo ya udhibiti wa kemikali hizo ambazo zinazodhibitiwa ambazo zina madhara mbalimbali katika jamii ikiwemo magonjwa, ongezeko la joto duniani na mabadiliko ya tabianchi.

“Tutaendelea kushirikiana na vyombo vya habari katika kuhakikisha elimu ya uhifadhi na utunzaji wa mazingira inaifikia jamii…Tunatambua mchango mkubwa wa JET kwani tangu kuanzishwa kwake mwaka 1991 imekuwa mstari wa mbele kuhamasisha jamii kutunza na kuhifadhi mazingira” amesema Mitawi.

Akifafanua zaidi Mitawi amesema ni takribani miaka 35 sasa tangu Jumuiya ya Kimataifa ipoamua kuchukua hatua mahsusi za kunusuru tabaka la ozoni katika kulinda afya ya binadamu na mazingira ambapo mwaka 1987 ilipitishwa Itifaki ya Montreal kuhusu udhibiti wa kemikali zinazomong'onyoa tabaka hilo.

“Lengo kuu la Itifaki hii ni kupunguza uzalishaji na matumizi ya kemikali zinazomong'onyoa tabaka la Ozoni….Nafasi ya vyombo vya habari ni kubwa katika kuelimisha jamii kuhusu athari ya matumizi ya kemikali hizi ambapo zimeleta athari mbalimbali ikiwemo mabadiliko ya tabianchi” amesema Mitawi.

Amesema katika jitihada za kuhifadhi tabaka la ozoni, Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais imeandaa na kutekeleza programu na shughuli mbalimbali ikiwemo kuendelea kuhimiza jamii kupunguza shughuli za kibinadamu ambazo zinasababisha mabadiliko ya tabianchi pamoja na kutoa mafunzo kwa Maafisa Forodha na Wasimamizi wa Sheria maeneo ya mipakani.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Mazingira, Ofisi ya Makamu wa Rais, Bi. Kemilembe Mutasa amesema juhudi mbalimbali zimeendelea kufanywa na Serikali katika Tabaka la Ozoni ikiwemo amesema katika kuelekea Siku ya Tabaka la Hifadhi ya Ozoni kutoa mafunzo kwa mafunzo mchundo na maafisa wa forodha na wasimamizi wa sheria katika maeneo ya mipakani.

“Tanzania sio mzalishaji wa kemikali hizi...Tumekuwa tukipokea kutoka nchi za nje..Tumeandaa kanuni, sera, sheria na miongozo mbalimbali katika kuelimisha jamii na pia Tumekuwa na mfululizo wa mafunzo haya kwa makundi mbalimbali ili kudhibiti kemikali hizi” amesema Kemilembe.

Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo, Bi. Mariam Mziwanda ameishukuru Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kuandaa mafunzo hayo na kutambua mchango wa vyombo vya habari katika kutoa elimu kuhusu udhibiti wa tabaka la ozoni katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

“Suala la usimamizi wa uhifadhi na utunzaji wa mazingira halipaswi kuachiwa Serikali pekee …Ni wajibu wetu sote kuunga mkono juhudi hizo…Tunaishukuru Ofisi ya Makamu wa Rais kutambua nafasi ya vyombo vya habari katika kufikisha elimu ya uhifadhi wa tabaka la ozoni kwa jamii” amesema Mariam.

Tarehe 16 Septemba kila mwaka, Tanzania huungana na Jumuiya ya Kimataifa kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Hifadhi ya Tabaka la Ozoni . Kauli mbiu ya Siku ya Kimataifa ya Hifadhi ya Tabaka la Ozoni mwaka 2023 ni “Hifadhi ya tabaka la ozoni na kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi”

Settings