Habari
Masauni: NEMC ina mengi ya kujivunia
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni amesema kuna kila sababu ya kujivunia mafanikio makubwa ndani Baraza La Taifa La Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) ikiwa inaelekea kutimiza miaka 40 tangu kuanzishwa kwake.
Mhe. Masauni amesema mafanikio hayo yanatokana na mchango mkubwa wa Bodi, uongozi pamoja na watumishi wote wa NEMC kwa namna ambavyo wanafanya kazi kwa ushirikiano katika kutimiza lengo.
Waziri Masauni ameyasema hayo wakati wa Kikao cha Bodi ya Wakurugenzi wa NEMC kilichofanyika Jijini Dar es Salaam, Mei 26, 2026 ambapo viongozi mbalimbali waliowahi kufanya kazi walipewa vyeti vya kuthamini mchango wao tangu kuanzishwa kwa Baraza hilo.
“Bado tuna deni kubwa kwa wananchi ili kuona tunapiga hatua zaidi ndio maana wakati nasoma bajeti iliahidi mambo mengi ambayo tunapaswa kuyatekeleza ili Tanzania iwe yenye mazingira bora.
“Natumaini kila mmoja akisimama vyema kwenye nafasi yake, basi miaka 40 ijayo mazingira yetu yatakuwa bora na salama kwa kuwa mwanzo wetu umeonekana kwenda vizuri hadi sasa,” amesema Mhe. Masauni.
Katika kikao hicho Mhe. Masauni aliambatana na Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais Mhe. Reuben Kwagilwa, Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Richard Muyungi pamoja na Naibu Katibu Mkuu (Mazingira), Ofisi ya Makamu wa Rais, Balozi Baraka Luvanda.



