Habari
Masauni aasa vijana kutumia fursa za mazingira
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni amesema vijana wanapaswa kutumia fursa zinazotolewa na Serikali kwa kukuza ubunifu, kuongeza bidii katika kazi, kutumia teknolojia na kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi hususan zilizo rafiki kwa Mazingira.
Mhe. Masauni amesema hayo katika Kongamano la Vijana lililofanyika jijini Dar es Salaam, Juni 2, 2026 ambalo ni sehemu ya Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani ambapo kilele chake kitaifa yanafanyika Juni 5, 2026 mkoani Dodoma.
Amesema, kongamano hilo ni jukwaa muhimu linalowaunganisha vijana na maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani kwa kuwapa nafasi ya kushiriki katika mijadala, kujifunza kutoka kwa wataalam, kubadilishana uzoefu na kuibua suluhisho bunifu zinazoweza kutekelezwa kwa vitendo katika jamii zao.
“Ninyi ndio nguvu kazi ya Taifa na nguzo muhimu katika mapambano dhidi ya uharibifu wa mazingira. Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, vijana ni zaidi ya asilimia 64 ya nguvu kazi ya Taifa. Hii ina maana kuwa mchango wenu ni muhimu sana katika kulinda mazingira, kukuza uchumi wa kijani na kuhakikisha maendeleo endelevu ya Taifa letu.



