Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Makamu wa Rais

Makamu wa Rais kumwakilisha Rais Mkutano wa Nane wa Nusu Mwaka wa AU

Oct, 03 2026

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius John Ndejembi, amesema Afrika ina sera, mikakati na makubaliano mazuri ya maendeleo, lakini sasa inapaswa kuongeza kasi ya utekelezaji ili rasilimali na fursa zilizopo barani humo ziweze kuleta manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi.

Makamu wa Rais amesema hayo leo, Oktoba 3, 2026, akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye Jukwaa la Biashara la Alamein, Afrika linalofanyika katika mji wa New Alamein Misri.

Akizungumza katika majadiliano ya ngazi ya juu katika mada inayohusu “Makubaliano Mapya ya Ukuaji wa Afrika katika Dunia yenye Misukosuko” (Africa’s New Growth Compact in a Turbulent World), Makamu wa Rais amesema katika mazingira ya sasa ya misukosuko ya uchumi na migogoro ya kikanda, Afrika inahitaji kuongeza uzalishaji, kujenga uchumi wenye uwezo wa kustahimili migogoro ya nje na kuhakikisha rasilimali zake zinatumika kuchochea maendeleo yenye manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi.

Amesisitiza umuhimu wa uwekezaji katika nishati na miundombinu kama msingi wa ukuaji mpya wa Afrika, akieleza uzoefu wa Tanzania katika kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati, ikiwemo Mradi wa Kufua Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP), wenye uwezo wa kuzalisha megawati 2,115 za umeme.

Amesema uwekezaji huo ni sehemu ya jitihada za Tanzania za kuongeza upatikanaji wa nishati ya uhakika kwa wananchi na shughuli za uzalishaji, huku nchi ikiwa na lengo la kufikia upatikanaji wa umeme kwa wote ifikapo mwaka 2050.

Aidha, Makamu wa Rais amesema kupitia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Tanzania imeweka mkazo katika maeneo ya kimkakati yanayolenga kuongeza uzalishaji na kuimarisha sekta ya nishati, ikiwemo matumizi ya gesi asilia na vyanzo vya nishati jadidifu, sambamba na kuboresha miundombinu inayowezesha shughuli za kiuchumi.

Makamu wa Rais amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi, uwekezaji unaovuka mipaka na kuunganisha uchumi wa nchi za Afrika ili kupunguza utegemezi wa masoko na mitaji kutoka nje ya bara.

Amesema Afrika inahitaji kujenga mazingira yatakayovutia mitaji ya sekta binafsi kuelekezwa katika miradi inayoongeza uzalishaji, ajira na thamani ya rasilimali za bara, sambamba na kuendeleza miradi ya kikanda inayounganisha nchi na masoko.

Akitolea mfano Tanzania, Ndejembi amesema nchi imeendelea kushirikiana na mataifa mbalimbali ya Afrika Mashariki katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati katika sekta za reli, mafuta, nishati na bandari, hatua inayochochea biashara na mtangamano wa kiuchumi katika ukanda huo.

Katika mjadala huo, Makamu wa Rais amesisitiza kuwa Afrika tayari ina sera, mipango na makubaliano mazuri, hivyo kinachohitajika sasa ni kuyatekeleza kwa vitendo kwa kubadili mitazamo, kuongeza ushirikiano, kuimarisha utashi wa kisiasa na kufanya maamuzi yanayoweka mbele maslahi ya wananchi wa Afrika.

Mkutano huo umefunguliwa na Rais wa Misri, Mhe. Abdel Fattah El-Sisi, na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Afrika, akiwemo Rais wa Burundi na Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU), Mhe. Évariste Ndayishimiye, pamoja na viongozi wa Taasisi za Bara la Afrika, Sekta Binafsi na Taasisi za Fedha.

Akizungumza katika ufunguzi wa mkutano huo, Rais wa Burundi na Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika, Mhe. Évariste Ndayishimiye, amesema Afrika ina utajiri mkubwa wa rasilimali asilia, ardhi ya kilimo, madini, vyanzo vya nishati, idadi kubwa ya vijana na soko kubwa, lakini changamoto iliyopo ni kugeuza rasilimali na fursa hizo kuwa matokeo halisi ya kiuchumi.

Ametoa wito kwa Serikali na wawekezaji kuongeza ushirikiano wa kiuchumi, uwekezaji na uzalishaji ili kufanikisha malengo ya Agenda 2063 ya Umoja wa Afrika.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Dangote Group, Aliko Dangote, amesema misukosuko inayoikabili dunia imeathiri pia uchumi wa Afrika, hivyo bara linapaswa kutumia rasilimali zake kujenga uwezo wa uzalishaji na kuimarisha uchumi wake.

Dangote amesisitiza umuhimu wa Afrika kuharakisha ukuaji wa viwanda na kuongeza thamani ya rasilimali zake ndani ya bara, badala ya kuendelea kuuza malighafi na baadaye kuagiza bidhaa zilizotengenezwa kutokana na malighafi hizo.

Alamein–Africa Business Forum imewakutanisha viongozi na maofisa waandamizi kutoka nchi mbalimbali za Afrika, viongozi wa taasisi za fedha za kikanda na kimataifa, wawekezaji, wafanyabiashara na wakuu wa kampuni kutoka ndani na nje ya bara.

Miongoni mwa viongozi wa taasisi wanaoshiriki ni Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika; Mkurugenzi Mtendaji wa AUDA-NEPAD, na Rais na Mwenyekiti wa Afreximbank. Jukwaa hilo linalenga kuimarisha biashara, uwekezaji na ushirikiano kati ya Serikali, Taasisi za Afrika na Sekta Binafsi ili kuchochea mtangamano na maendeleo ya uchumi wa Bara la Afrika.

Habari

Settings