Makamu wa Rais awashukuru Watanzania kwa kumfariji msiba wa dada yake

Aug, 30 2023

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amewashukuru watanzania na waombolezaji wote walioungana na familia katika maombolezo na mazishi ya dada yake Bi. Maria Isdor Nzabhayanga.

Makamu wa Rais ametoa shukrani hizo mara baada ya mazishi ya Bi. Maria Isdor Nzabhayanga yaliofanyika katika Kijiji cha kipalapala mkoani Tabora. Amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na serikali nzima kwa maneno ya faraja na upendo wakati wote wa msiba huo sambamba na kuwashukuru viongozi wa dini, watoa huduma za afya na majirani wa Bi Maria kwa mchango wao waliotoa wakati wa uhai wake.

Awali akitoa salamu za rambirambi kwa niaba ya serikali, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa amesema wanatoa pole na kuungana na familia pamoja na wote waliokuwa karibu na Bi Maria wakati wa Maisha yake duniani katika kipindi hiki kigumu cha majonzi.

Waziri Mkuu amesema inapaswa kuenzi mazuri aliofanya na kuyaacha wakati wa uhai wake pamoja na kumuombea kwa Mwenyezi Mungu ili aweze kupumzika kwa amani.

Mazishi hayo yamehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, wabunge, viongozi wa dini, vyama vya siasa na wananchi kutoka maeneo mbalimbali.

Settings