Habari
Makamu wa Rais awasaihi viongozi wa dini kufundisha maadili
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi amewasihi Viongozi wa Dini kuendelea kuwekeza katika kufundisha maadili mema kwa kizazi cha sasa ili kuwa na Taifa zuri baadaye.
Makamu wa Rais amesema hayo wakati aliposhiriki Futari iliyoandaliwa na Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT) iliyohusisha Viongozi wa Dini na Wadau wa Amani nchini, iliyofanyika Jijini Dar es Salaam tarehe 19 Machi 2026. Amesema ni vema kutoa kipaumbele cha pekee katika eneo la maadili kwa kuwa kuharibika kwa malezi ya sasa ni kuharibu kizazi kijacho.
Amesema kumekua na changamoto katika maadili na makuzi ya watoto, hivyo Viongozi wa Dini watakapoweka kipaumbele katika kufundisha maadili kwa waumini watakuwa wametoa mchango mkubwa kwa jamii na Taifa kwa ujumla.
Makamu wa Rais, ameipongeza Jumuiya ya Maridhiano na Amani (JMAT) kwa kazi kubwa waliyofanya ya kuimarisha mahusiano ya dini mbalimbali hapa nchini. Amesema Serikali inatambua na kuthamini kazi inayofanya Jumuiya hiyo ikiwa ni pamoja na kuelimisha wajibu wa viongozi wa dini na wajibu waumini katika kutambua nafasi zao kuleta amani katika nchini.
Makamu wa Rais amesema Tanzania inajivunia kuwa nchi ambayo wananchi wake wana ushirikiano bila kujali dini zao, hivyo ni muhimu kuendelea kusimamia ushirikiano huo.
Aidha, amesema ni muhimu kuimarisha mambo yote yaliyofanywa kipindi cha toba yaani Mwezi Mtukufu wa Ramadhan na kwaresma na kuyaendeleza.
Futari hiyo imehudhuriwa na Viongozi wa dini mbalimbali, Mabalozi wanaowakilisha nchi zao Tanzania, Wakuu wa Taasisi mbalimbali, Wasanii, pamoja na wadau wa amani nchini.



