Habari
Makamu wa Rais asisitiza, Sitta alituachia dira ya uongozi, tuiishi
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, amewataka viongozi kuuenzi urithi wa Hayati Samuel John Sitta kwa kuishi misingi ya uadilifu, uwajibikaji na kujenga Taasisi imara, akisisitiza kuwa historia yake inapaswa kuwa mwongozo wa utumishi kwa Taifa.
Makamu wa Rais ametoa ujumbe huo, leo, Novemba 3, 2026, alipomwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye kumbukizi ya miaka 10 ya kifo cha Hayati Samuel Sitta na uzinduzi wa kitabu cha maisha na safari yake ya uongozi, iliyofanyika katika Ukumbi wa Pius Msekwa, Bungeni Jijini Dodoma.
Amesema Hayati Sitta anakumbukwa kwa alama alizoacha katika maisha ya watu na taasisi, maono yake na msimamo wa kutanguliza maslahi ya Taifa.
Akizungumzia mchango wake akiwa Spika wa Bunge, amesema alisimama kidete kulinda hadhi ya chombo hicho, uadilifu wa taasisi za umma na heshima kwa taratibu na kanuni
Ameeleza kuwa Hayati Samuel Sitta alizitazama taratibu hizo kama dhamana ya haki na nguzo ya uhalali wa kidemokrasia, huku akiamini kwamba Taifa lenye nguvu hujengwa na taasisi imara. “Uongozi wa kweli si njia ya kujitafutia umaarufu, hadhi au manufaa binafsi bali ni wajibu, utumishi, na ni kujitoa kwa ajili ya wengine,” amesema.
Amesisitiza kuwa wajibu wa viongozi wa sasa ni kuhifadhi uzoefu na mafunzo ya Sitta na kuyatafsiri katika namna wanavyotimiza majukumu yao, ili urithi huo uendelee kuwa na manufaa kwa wananchi.
Kwa mujibu wa Makamu wa Rais, kitabu hicho kinabeba sehemu ya kumbukumbu ya Taifa na historia yake ya kidemokrasia, hivyo wasomaji wake watapata mafunzo kuhusu utumishi wa umma, umuhimu wa taasisi na kujitolea kunakohitajika katika kuijenga nchi.
Amewahimiza viongozi, hususan vijana, wanafunzi na Watanzania wote kukisoma kitabu hicho ili kujizolea maarifa “Taifa linalokumbuka wajenzi wake huhifadhi utambulisho wake; Taifa linaloheshimu utumishi huwahamasisha wengine kutumikia.” Alisisitiza
Makamu wa Rais alihitimisha kwa kutambua mchango mkubwa wa familia ya Hayati Samwel Sitta, akisema utumishi wa viongozi hubebwa pia na uvumilivu, msaada na kujitolea kwa familia zao, na kuishukuru familia ya Sitta kwa mchango wake katika safari ya kulitumikia Taifa.
Awali, akimkaribisha Makamu wa Rais, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mussa Azan Zungu, amesema Hayati Samuel Sitta ataendelea kukumbukwa kwa uchapakazi, uzalendo mkubwa na alama alizoacha, hasa alipokuwa Spika.
Hayati Samuel John Sitta, aliyekuwa Mbunge wa Urambo na Spika wa nne wa Bunge, alilitumikia Taifa kwa zaidi ya miongo minne katika nyadhifa mbalimbali, kuanzia Serikali ya Awamu ya Kwanza chini ya Hayati Mwalimu Julius Nyerere. Miongoni mwa majukumu aliyowahi kubeba ni uwaziri, ukuu wa Mkoa, uongozi wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania na uenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba.
Kwa upande wake, mjane wa Hayati Samuel Sitta, Mhe. Margaret Sitta, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Urambo, amemwelezea kuwa baba mahiri, mzalendo na mpenda haki aliyethamini ubunifu na uwajibikaji. Amesema aliishi kwa vitendo falsafa ya viwango na kazi, akiwa muumini mkubwa wa mabadiliko.
Kitabu kilichozinduliwa chenye kurasa 217 kinaangazia historia ya uongozi wa Hayati Samuel Sitta, maono yake kwa Taifa na falsafa zilizoyaongoza maisha yake. Pia kinaeleza mafundisho aliyoyapata katika safari ya utumishi, falsafa za Mwalimu Nyerere na namna alivyoziishi katika kutekeleza majukumu yake.
Hafla hiyo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Waziri Mkuu Mstaafu John Malecela, Spika Mstaafu Anna Makinda, Familia ya marehemu Sitta, Mawaziri, Wabunge na watumishi wakiowahi kufanya naye kazi.
Uzinduzi huo umeweka kumbukumbu za maisha yake mikononi mwa kizazi cha sasa na kijacho, huku Viongozi wakitakiwa kuyafanya mafunzo yaliyohifadhiwa katika kurasa hizo yaonekane katika matendo ya kila siku ya kulitumikia Taifa.



