Makamu wa Rais ashiriki Mkutano wa SADC

Aug, 17 2023

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango leo tarehe 17 Agosti 2023 amemwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. SamiaSuluhu Hassan kwenye Mkutano wa 43 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini Mwa Afrika (SADC) uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Hoteli ya Intercontinental, Jijini Luanda nchini Angola.

Mkutano huo uliobeba kaulimbiu ya “Umuhimu wa Rasilimali Fedha na Rasilimali Watu katika kuendeleza Viwanda na Uchumi” umehudhuriwa na viongozi Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya hiyo, Mawaziri, Viongozi wa Kisekta pamoja na Wakuu wa Majeshi.

Baadhi ya masuala yaliyojadiliwa katika mkutano huo ni pamoja na uendelezaji viwanda kwa kuhakikisha uongezaji thamani wa bidhaa unafanyika ndani ya nchi wanachama ili kuongeza ajira na mapato kwa mataifa husika.

Pia, Tanzania imesisitiza umuhimu wa usalama wa chakula pamoja na umuhimu wa kutafuta amani kwa nchi za Msumbiji na Jamhuri ya Kidemokrasiaya Kongo.

Katika Mkutano huo, Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Mheshimiwa Felix Tshisekedi amekabidhi Uenyekiti wa SADC kwa Rais wa Jamhuriya Angola Mheshimiwa João Lourenço. Pia, Rais wa Namibia Dkt. Hage Geingob amekabidhi Uenyekiti wa Asasi ya Ushirikiano katika Masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini Mwa Afrika (SADC Organ Troika) kwa Rais wa Zambia Mheshimiwa Hakainde Hichilema.

Mkutano huo, umetoa zawadi mbalimbali kwa washindi wa shule za sekondari washindano la insha la Jumuiya ya Maendeleo Kusini Mwa Afrika (SADC) ambapo Mwanafunzi Hollo Kadala wa shule ya sekondari Msalato kutoka nchini Tanzania ameshinda nafasi ya tatu.

Mkutano wa 43 wa Wakuu wa Nchi na Serikali umetanguliwa na mkutano wa Kamati ya Baraza la Mawaziri la Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) uliofanyika tarehe 13–14 Agosti 2023.

Settings