Makamu wa Rais akutana na mtafiti wa sokwe Hifadhi ya Gombe

Jul, 09 2024

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amekutana na kufanya mazungumzo na Mwana Anthropolojia na Mwana Primatolojia aliyetafiti kuhusu Maisha ya Sokwe katika Hifadhi ya Taifa ya Gombe mkoani Kigoma Bi. Jane Goodall, mazungumzo yaliyofanyika Ikulu ndogo Kigoma.

Katika mazungumzo hayo, Makamu wa Rais amempongeza na kumshukuru Bi. Goodall kwa mchango wake katika uhifadhi hapa nchini na kuitangaza Hifadhi ya Gombe na mkoa wa Kigoma kwa ujumla.

Akizungumza na Wananchi wa Kigoma wakati akifungua barabara iliyopewa jina la mtafiti Bi. Jane Goodall inayoelekea eneo la kibirizi ziwani kwenda Hifadhi ya Taifa ya Gombe, Makamu wa Rais amesema Bi. Goodall ametoa mchango mkubwa katika kutoa elimu ya viumbe na mwalimu muhimu wa uhifadhi.

Amewahimiza vijana na kuwasisitiza kujifunza zaidi elimu ya hifadhi ya misitu na mazingira kwa ujumla. Makamu wa Rais ameupongeza uongozi wa Manispaa ya Kigoma Ujiji kwa kutambua mchango wa Mtafiti huyo na kuweka alama ya barabara itakayokumbuka mchango wake.

Makamu wa Rais anaendelea na Ziara mkoani Kigoma yenye lengo la kukagua miradi ya maendeleo pamoja na kusikiliza changamoto mbalimbali za wananchi.

Settings