Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema Tanzania imedhamiria kuhakikisha usimamizi endelevu wa mkondo wa Pemba pamoja na ikolojia ya baharini kwa ujumla.
Makamu wa Rais amesema hayo wakati akifungua Mkutano wa pembezoni uliyohusu “Kujenga Uchumi wa Buluu Imara katika Mkondo wa Bahari wa Pemba: Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Bahari kwa Maisha Endelevu na Mabadiliko ya Tabianchi” uliyofanyika kando ya Mkutano wa Tatu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Bahari unaofanyika Jijini Nice nchini Ufaransa.
Amesema dhamira ya nchi ni kuhakikisha Uchumi wa Buluu unakuwa kielelezo cha ukuaji jumuishi, utunzaji wa mazingira na ustahimilivu wa muda mrefu. Amesisitiza umuhimu wa kufanya kazi pamoja katika kuchukua hatua za haraka ili kulinda Bahari kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.
Makamu wa Rais amesema Tanzania inachukua hatua mbalimbali katika kukabiliana na hatari zinazoikumba ikolojia ya Bahari ili kuhakikisha mkondo wa Pemba unakua himilivu pamoja na uendelevu wa mazingira kwa muda mrefu.
Ametaja hatua hizo ni pamoja na kuimarisha uhifadhi wa Bahari kupitia usimamizi imara na uongezwaji wa maeneo ya hifadhi ya bahari (MPAs), ambapo amesema kwamba maeneo mawili mapya ya uhifadhi kisiwani Pemba yako katika hatua za mwisho za kutangazwa, hivyo kuimarisha azma ya nchi ya kulinda urithi wa kipekee wa bahari.
Halikadhalika, Makamu wa Rais amesema Tanzania inahakikisha ushiriki wa jamii katika uhifadhi wa bahari kwa maendeleo ya uchumi wa buluu ambapo inahusisha ufanyaji kazi kwa pamoja ili kuhakikisha kwamba juhudi za maendeleo ya baharini na pwani ni jumuishi, zenye usawa na endelevu. Pia kusaidia njia mbadala za maisha, kuimarisha minyororo ya thamani kwa wavuvi wadogo na kufungua fursa za ustawi kwa jamii za pwani sambamba na kuhifadhi mfumo wa ikolojia.
Vilevile, Makamu wa Rais Tanzania inaendeleza ushirikiano wa kimataifa kwa kutambua kwamba ulinzi wa bahari ni shirikishi. Amesema kupitia ushirikiano na taasisi za fedha, mashirika yasiyo ya kiserikali, mashirika ya utafiti na sekta binafsi, imesaidia katika kuhamasisha matumizi ya sayansi, upatikanaji fedha na uvumbuzi ili kuongeza matokeo chanya na kujenga uwezo wa ndani.
Mkondo wa Pemba ni eneo linalopatikana kati ya Tanzania Bara mkoa wa Tanga na Kisiwa cha Pemba,Zanzibar ni eneo muhimu lenye ikolojia muhimu katika sekta ya bahari. Linajumuisha miamba ya matumbawe, nyasi za bahari na mifumo ya ikolojia ya mikoko ambayo inachagiza sekta ya uvuvi nchini na kusaidia jamii za pwani na hutumika kama kinga dhidi ya athari zinazoongezeka kutokana na mabadiliko ya tabianchi.
Mkutano huo wa pembezoni ambao umelenga kuonyesha mafanikio ya Tanzania katika usimamizi jumuishi wa Bahari unaoongozwa na jamii, umewashirikisha wadau mbalimbali wa bahari na mazingira kutoka mataifa mbalimbali Duniani.