Makamu wa Rais afungua Hospitali ya Wilaya Karatu

May, 16 2023

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango leo tarehe 16 Mei 2023 akiwa ziarani Mkoani Arusha amefungua rasmi Hospitali ya Wilaya ya Karatu iliogharimu shilingi bilioni 3.37.

Akihutubia mara baada ya kufungua hospitali hiyo, Makamu wa Rais amesema serikali itaendelea kuhakikisha huduma bora za afya zinasogezwa Jirani na wananchi pamoja na kuimarisha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba katika kila vituo vya kutolea huduma za afya.

Ameagiza uongozi wa Wilaya na hospitali kusimamia kwa uaminifu dawa zinazoletwa na serikali kwa ajili ya matumizi ya wananchi ambapo kinyume na hapo serikali itachukua hatua kali za kisheria dhidi ya kiongozi yeyote atakayebainika kukiuka sheria na miongozo iliyotolewa na serikali ya uendeshaji wa maduka ya dawa ya hospitali.

Makamu wa Rais amesema hospitali hiyo inalenga pia kusaidia watalii kuwa na uhakika wa kupata huduma ya kwanza na ya dharura kwa haraka katika mazingira salama pale itakapo hitajika. Pia ametoa wito kwa wananchi wa Karatu kutunza hospitali hiyo ili iweze kusaidia wananchi kwa miaka mingi ijayo.

Vilevile Makamu wa Rais ametoa wito kwa madaktari na wahudumu wa afya katika hospitali hiyo, kuwahudumia wananchi kwa upendo na uadilifu. Amesema Serikali itaendelea kuhakikisha vitendea kazi vinapatikana ili majengo yote yaanze kufanya kazi kama ilivyokusudiwa.

Pia ametoa wito kwa wananchi, kushirikiana na uongozi wa Wilaya ili kuleta maendeleo katika Wilaya hiyo na kuagiza viongozi katika ngazi ya vijiji na kata kuendelea kuimarisha kamati za afya za vijiji na kata ili zisaidie kuhamasisha afya ya wananchi.

Settings