Makamu wa Rais afanya mazungumzo na Rais wa Cuba

Mar, 01 2023

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango leo Machi 01, 2023 amekutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais wa Cuba Mhe. Salvado Valdés Mesa mazungumzo yao yaliofanyika katika Mji wa Baku nchini Azerbaijan.

Katika mazungumzo hayo Makamu Rais Dkt. Mpango amesema Tanzania na Cuba zimeendelea kuwa na uhusiano thabiti katika sekta mbalimbali za maendeleo kama vile Afya, Elimu, Viwanda na Biashara. Pia ameishukuru nchi ya Cuba kwa kuendelea kushirikiana na Tanzania katika utoaji wa mafunzo hususani kwa kutoa ufadhili kwa wanafunzi wa fani ya udaktari, michezo na fani nyinginezo pamoja na wataalamu kutoka nchi hiyo kufanya kazi katika hospitali mbalimbali nchini Tanzania.

Makamu wa Rais amesema Tanzania itaendeleza ushirikiano mzuri baina ya mataifa hayo mawili ulioasisiwa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere na Rais Fidel Castro wa Cuba, uhusiano uliosaidia kwa kiasi kikubwa katika ukombozi wa nchi za kusini mwa Afrika wakati wa kupigani uhuru. Amesema kwa sasa uhusiano huo unaweza kuongezwa zaidi katika sekta za kilimo na utalii ambazo zitakuwa na manufaa kwa mataifa yote mawili.

Kwa upande wake Makamu wa Rais wa Cuba mheshimiwa Salvado Valdés Mesa amesema uhusiano uliopo wa muda mrefu baina ya Tanzania na Cuba unathibitisha urafiki, umoja na ushirikiano wa kihistoria uliodumu katika mataifa hayo. Pia ameishukuru Tanzania kwa kuendelea kuiunga mkono Cuba katika masuala mbalimbali katika jumuiya za kimataifa pamoja na nia yake ya dhati ya kuendelea kushirikiana na Cuba.

Ameongeza kwamba Cuba itaendelea kusikiliza mahitaji ya Tanzania yanayolenga kuongeza ushirikiano baina ya mataifa hayo mawili hususani katika sekta ya afya na nyinginezo. Mheshimiwa Mesa amesema Cuba ipo tayari kutoa msaada wa kitaalamu katika uzalishaji wa sukari , uzalishaji wa dawa pamoja na utengenezaji chanjo zikiwemo chanjo za watoto na Uviko 19.

Katika hatua nyingine Makamu wa Rais amekutana na kufanya mazungumzo na Naibu Waziri Mkuu wa Azerbaijan Mheshimiwa Shahin Mustafayev,Mazungumzo yaliofanyika katika Mji wa Baku nchini Azerbaijan.

Katika mazungumzo hayo wamejadili masuala mbalimbali ya ushirikiano katika sekta ya nishati ya mafuta nagesi, elimu, utalii , biashara na uwekezaji.

Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango yupo nchini Azerbaijan kumwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa Nchi Zisizofungamana na Upande Wowote (Non – Aligned Movement) unaotarajiwa kufanyika tarehe 02 Machi 2023 nchini humo.

Settings