Makamu wa Pili wa Rais aeleza umuhimu wa Mkutano wa AGN

Apr, 28 2025

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amesema Mkutano wa Kundi la Majadiliano la Afrika kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (AGN) ni muhimu kwa Tanzania na Afrika kwa ujumla kwani utajadili mambo mbalimbali ikiwemo matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Amesema mkutano huo pia, utawaunganisha Waafrika zaidi ya milioni 300 katika matumizi ya nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2030 ili kuhifadhi mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi Barani Afrika.

Mhe. Hemed amesema hayo wakati akifungua Mkutano wa Kundi la Majadiliano la Afrika (AGN) kwa niaba ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango katika Ukumbi wa Hotel Verde Mtoni, Zanzibar leo tarehe 28 Aprili 2025.

Kadhalika, Makamu wa Pili wa Rais amewataka washiriki huo kuhakikisha mijadala yao inalenga zaidi kuangalia fursa na changamoto ambazo Afrika inakabiliana nazo hivyo ni muhimu wawetumie mkutano huo kuweka vipaumbele muhimu vya kimkakati vitakavyoisaidia Afrika kupambana na mabadiliko ya tabianchi.

Aidha, amesema athari za mabadilko ya tabianchi zimekuwa zikiongezeka na kuathiri nchi nyingi za Afrika na kusababisha kupungua kwa fedha za hali ya hewa jambo linaliochangia wazalishaji wakubwa wa gesijoto kujiondoa kutokana na changamoto hiyo.

Mhe. Hemed amesema pamoja na kuwa Afrika ina utajiri wa asili kama ukiwemo madini muhimu kwa teknolojia ya kijani kibichi bado zaidi ya Waafrika milioni 600 hawana uwezo wa kupata nishati safi na nafuu jambo ambalo halikubaliki hivyo jitihada za haraka zinapaswa.


Ameongeza kuwa Afrika inapaswa kutumia rasilimali zake ili kuvutia wawekezaji hasa katika nishati ya kijani na teknolojia zinazosukuma maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Sanjari na hilo, ametoa wito kwa washiriki wa mkutano huo kuangalia namna bora za udhibiti na uhifadhi wa mazingira kupitia mikataba na miongozo mbali mbali ya Kimataifa ambayo itainufaisha zaidi Bara la Afrika katka suala la mazingira.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa wa Zanzibar Mhe. Harusi Said Suleiman amesema kufanyika kwa mkutano huo kunaonesha umuhimu unaowekwa na AGN katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuhakikisha kuwa Afrika iko salama kimazingira.

Amesema mkutano huo unalenga kuimarisha na kufanya ushawishi kwa nchi za Afrika katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuweka mikakati na maadhimio thabiti yenye kuisaidia Afrika kuepukana na changamoto mbali mbali za kimazingira na kuweza kufika malengo waliyojiwekea.

Naye Mwenyekiti wa Mkutano AGN Dkt. Richard Muyungi amesema mkutano huo utajadili na kutoa maamuzi juu ya masuala ya tabianchi namna yatakavyoshughulikiwa kwa mwaka mzima pamoja na mambo mengine ya msingi ambayo Afrika inataka yasimamiwe katika kuelekea mkutano mkubwa wa nchi zote duniani na mkataba wa mabadiliko ya tabianchi.

Dkt. Muyungi amesema mkutano huo utazingatia mambo muhimu yakiwemo kuweka mikakati ya kupunguza gesi joto na kuongeza uvumilivu wa mabadilo ya tabianchi.

Pia, amesema washiriki wa mkutano wana jukumu la kuhakikisha Afrika inatumia nishati za mpito ambayo itaisaidia Afrika katika dunia iliyo salama sanjari na kuachana na matumizi ya nishati za mafuta lengo ni kuhakikisha Afrika inalinda na kuhifadhi mazingira.

Settings