Habari
Kwagilwa ashiriki kikao cha Kamati za Bunge
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Reuben Kwagilwa ameshiriki kikao cha Kamati za Kudumu za Bunge za Utawala, Katiba na Sheria pamoja na Maji na Mazingira ambapo Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) iliwasilisha taarifa ya usimamizi wa taka ngumu, fursa za kiuchumi zinazotokana na taka na mapendekezo ya mabadiliko ya Sheria yatakayowezesha kuanzishwa kwa Mamlaka ya Taifa ya Usimamizi wa Mazingira (NEMA).
Katika kikao hicho chini ya Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira Mhe. Jackson Kiswaga, wajumbe walipokea taarifa hiyo iliyojikita pia katika kuelezea umuhimu wa kuimarisha usimamizi wa taka ngumu ili kulinda afya ya jamii na mazingira.
Katika mkakati huo taka zikitambuliwa kama rasilimali zinazoweza kuzalisha fursa za kiuchumi kupitia urejelezaji na uchakataji.
Ilielezwa kuwa kuanzishwa kwa NEMA kunalenga kuimarisha uwezo wa kisheria wa kusimamia na kudhibiti masuala ya mazingira, pamoja na kurahisisha michakato ya biashara na uwekezaji bila kuathiri matakwa ya kisheria ya utunzaji wa mazingira.
Akizungumza baada ya kikao hicho, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt. Immaculate Semesi alisema mabadiliko ya Sheria yanayopendekezwa yanalenga kuiwezesha Taasisi kuwa Mamlaka kamili inayoendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, kwa kuwezesha biashara na uwekezaji na kukuza uchumi endelevu na rafiki kwa mazingira.
Aliongeza kuwa mabadiliko hayo yanahusisha kubadilika kwa jina kutoka NEMC kwenda NEMA na kuimarisha vipengele vya kisheria ili Taasisi iwe mwezeshaji badala ya kikwazo kwa wawekezaji, hususan katika kutimiza masharti na kupata vibali vinavyohitajika kwa mujibu wa sheria.



