Serikali kuwakutanisha wawekezaji wa pembezoni mwa barabara kukijanisha nchi

Jun, 11 2024

Serikali imesema ina mpango wa kukutana na wamiliki na wawekezaji wa maeneo yaliyo pembezoni mwa barabara ili kuweka mkakati wa pamoja wa upandaji miti na bustani za maua ili kuendelea kukijanisha nchi.


Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo amesema hayo katika kikao cha pamoja na Waziri wa Ujenzi Mhe. Innocent Bashungwa leo Juni 11, 2024 jijini Dodoma.

Kikao hicho viongozi hao na wataalamu wamejadili kuhusu Mradi wa Green Solution Project (GSP) unaofadhiliwa na Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB) kupitia ujenzi wa barabara ya mzunguko wa Jiji la Dodoma yenye urefu wa km 112.3.

Dkt. Jafo ameipongeza Wizara ya Ujenzi kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kwa zoezi la upandaji miti na kuitunza hususan katika barabara Chimwaga- Ihumwa JCT jijini Dodoma.

Akizungumzia kuhusu mradi huo, Waziri Bashungwa amesema Serikali itatumia shilingi bilioni 12 katika utekelezaji wa mradi wa kukijanisha Dodoma ikiwemo kupanda miti na maua katika hifadhi za barabara ili kutunza mazingira na kupendezesha mandhari ya jiji hilo.

Amesema timu za wataalamu wa Ofisi ya Makamu wa Rais na Wizara ya Ujenzi na taasisi zake zikishirikiana na kujadili suala la utunzaji wa mazingira hususan Dodoma watakuja na mikakati bora ya utekelezaji wa mradi huu.


Mhe. Bashungwa ameongeza kuwa kuanza kwa utekelezaji wa mradi huo kutafungua mawanda mapana kwa Serikali kutafuta wadau wa maendeleo watakaoshirikiana na Serikali kukijanisha maeneo mbalimbali nchini.

Hivyo, amemuagiza Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi kuisimamia TANROADS kuandaa usanifu na upembuzi yakinifu ambao hautaathiriwa na mabadiliko na uboreshaji wa miundombinu ya barabara ikiwemo upanuzi wa barabara ambao umekuwa ukisababisa ukataji wa miti ambayo imepandwa hivi karibuni.

Settings