​Katibu Mkuu Maganga akutana na wadau wa chupa za plastiki

Apr, 13 2021

Makampuni yanayozalisha bidhaa zinazofungasha chupa za plastiki zimepewa wiki moja kuandaa mikakati inayotekelezeka ya muda mfupi na mrefu itakayoonesha udhibiti wa chupa za plastiki wanazozizalisha na kuiwasilisha katika Ofisi ya Makamu wa Rais Aprili 20, 2021.

Agizo hilo limetolewa Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Bi. Mary Maganga wakati akifungua Kikao cha Wadau wanaojihusisha na shughuli za uzalishaji wa bidhaa zinazofungashwa kwa chupa za plastiki za rangi kilichofanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Makamu wa Rais, MtumbaAprili 13, 2021 jijini Dodoma.

Maganga alibainisha kuwa uchafuzi wa mazingira utakanao na chupa za plastiki zenye rangi umekuwa changamoto nchini. Aidha, katika kukabiliana na changamoto hizo kuna haja ya wazalishaji kutimiza wajibu wao wa kuziondosha katika mazingira ikiwemo kuzirejeleza kama Sheria ya Mazingira inavyoelekeza.

“Kutokana na umuhimu wa udhibiti wa taka za plastiki tunao wajibu wa kuungana pamoja ili kuwa na juhudi za pamoja katika kukabiliana na changamoto za udhibiti wa taka zitokanazo na plastiki kama Kanuni ya 4 ya Kanuni za Usimamizi wa taka ngumu za mwaka 2009 chini ya Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004 zinavyoelekeza,” alisema.

Hivyo kwa mujibu wa kanuni hizo ni kuwa mzalishaji anao wajibu wa kuondosha kwenye mazingira taka zitokanazo na bidhaa anazozalisha (Extended Producer Responsibility).

Katibu Mkuu Maganga alifafanua kuwa pamoja na jitihada za kuziondosha chupa hizo katika mazingira bado kumekuwa na changamoto ya kukosekana kwa makampuni ya kutosha yanayojishughulisha na urejelezaji wa chupa hizo.

Kutokana na changamoto hiyo alisema chupa hizo zimeendelea kuzagaa katika mazingira yetu na hivyo kuchangia uchafuzi wa mazingira ikilinganishwa na chupa zisizo na rangi.

“Natoa wito kwa jamii kukabiliana na changamoto za udhibiti wa taka zitokanazo na plastiki ambapo mzalishaji ana wajibu wa kuondosha kwenye mazingira taka zitokanazo na bidhaa anazozalisha,” alisisitiza Maganga.

Kikao hicho kimeshirikisha wawakilishi kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), mwakilishi kutoka Shirikisho la Wenye Viwanda (CTI) na wawaskilishi wa wamiliki wa viwanda.

Settings