Habari
Kamati ya Bunge yaipa kongole Ofisi ya Makamu wa Rais kwa utekelezaji wa miradi
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria leo Machi 09, 2026 imeipongeza Ofisi ya Makamu wa Rais kwa utekelezaji na usimamizi mzuri wa miradi ya mazingira.
Pongezi hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa kamati hiyo Mhe. Dkt. Damas Ndumaro wakati wa kikao cha kupokea na kujadili taarifa ya miradi iliyotengewa fedha mwaka 2025/26, kilichofanyika kwenye ofisi za Bunge jijini Dodoma.
Akiendelea kutoa pongezi hizo, Dkt. Ndumbaro ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini alisema kuwa utekelezaji mzuri wa miradi hiyo uwe chachu kwa wizara na taasisi zingine.
“Kwa kweli Ofisi ya Makamu wa Rais sisi letu leo ni pongezi na tunaomba mtufikishie salamu zetu kwa Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Makamu wa Rais, Mheshimiwa Waziri Mkuu na tunatamani wizara zingine ziige kutoka kwenu,“ alisema Dkt. Ndumbaro.
Awali akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa miradi iliyotengewa fedha kwa mwaka 2025/26, Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Festo Dugange alisema Ofisi hiyo imeendelea kuimarisha miundombinu yake kwa kujenga na kukarabati majengo.
Alisema lengo la miradi hiyo ni kuongeza ufanisi wa utendaji kazi kwa Watumishi wa Umma na kumuwezesha Makamu wa Rais kutekeleza majukumu yake ya kikazi kwa ufanisi.
Pia, Dkt. Dugange aliileza Kamati kuwa Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais itaendelea kuboresha mazingira ya watumishi ili kuiwezesha Ofisi kutekeleza kwa ufanisi majukumu yake.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Richard Muyungi, akiwasilisha taarifa ya ujenzi wa jengo la Ofisi ya Makamu wa Rais katika Mji wa Serikali Mtumba, Dodoma alisema utekelezaji huo umefikia asilimia 94.5.
Alisema kazi zilizobaki ni za umaliziaji wa ndani na nje na kuweka mifumo ikiwemo umeme wa kudumu na mfumo wa TEHAMA na mfumo wa maji safi ili kuwezesha matumizi ya jengo.



