Habari
Dkt Muyungi: Michezo ni uchumi
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Richard Muyungi amewahimiza wananchi kutenga muda wao na kushiriki katika michezo na mazoezi ya viungo ili kujijenga kiafya na kiakili.
Amesema hayo wakati akizungumza na watumishi wa Ofisi ya Makamu wa Rais mara baada ya kushiriki mazoezi ya viungo na mbio fupi yaliyofanyika jijini Dodoma leo Oktoba 31, 2026.
Dkt. Muyungi amesema kushiriki katika michezo si tu unajenga afya peke yake bali unaweza kujipatia kipato hususan unaposhiriki katika mashindano mbalimbali ndani na nje ya nchi.
Kwa mantiki hiyo kupitia michezo mbalimbali ikiwemo riadha, mpira wa miguu na mingineyo washiriki wanapofanya vizuri hutunukiwa zawadi zikiwemo medali au fedha taslimu hivyo huijiongezea kipato na uchumi wa taifa kwa ujumla.
Halikadhalika, Dkt. Muyungi aliwapongeza watumishi wa ofisi hiyo kwa kushiriki kikamilifu katika michezo hatua iliyochangia kuwepo na timu ya mchezo wa netiboli ambayo imefanya vizuri na kufanikiwa kuingia katika mashindano ya ligi daraja la kwanza ya mchezo huo nchini.
“Hivi sasa timu yetu ya netiboli inasikika nchi nzima na niwahakikishie itachukua kombe na yote haya ni kutokana na umoja wetu lazima tushirikiane kwani kupitia michezo tunaondoa uchovu wa kazi za wiki nzima na kujenga afya,“ alisema.
Aliongeza kuwa michezo ni sehemu ya kujenga umoja na mshikamano miongoni mwa wananchi ambapo unawakutanisha wananchi wa Tanzaia Bara na Zanzibar hasa ukizingatia Ofisi ya Makamu wa Rais ina jukumu la kuratibu Muungano.
Awali akizungumza baada ya mazoezi hayo, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimaliwatu Ofisi ya Makamau wa Rais Bi. Adela Mkude alimshukuru Katibu Mkuu kwa kutenga muda wake na kushiriki mazoezi hayo.
Ofisi ya Makamu wa Rais imejiwekea utaratibu kwa watumishi wake kukutana na kufanya mazoezi na viungo, kukimbia mbio fupi na michezo mbalimbali ili kujenga afya ya mwili na kiakili.



