Dkt. Mpango: Serikali ina dhamira ya kukuza uwekezaji

Sep, 23 2023

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema serikali ya Tanzania ina dhamira ya dhati ya kushirikiana na kufanya kazi kwa karibu na jumuiya ya wafanyabiashara wa ndani ya nchi na wale wa kimataifa ili kukuza uwekezaji wa sekta binafsi.

Makamu wa Rais amesema hayo wakati alipofanya mazungumzo na Taasisi ya Kimkakati kwa Biashara za Kimataifa na Serikali ya nchini Marekani (BCIU), mazungumzo yaliyofanyika Jijini New York. Amesema nchini Tanzania sekta binafsi ni mshirika mkuu wa maendeleo na taifa lipo tayari kwaajili ya biashara hivyo amewakaribisha wafanyabishara hao kuwekeza Tanzania na kutumia fursa zilizopo ili kuiwezesha nchi kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu (SDGs).

Makamu wa Rais amesema Tanzania ni nchi yenye mazingira mazuri zaidi ya uwekezaji kusini mwa jangwa la sahara ikiwa na kasi ya ukuaji kiuchumi, amani, miundombinu ya nishati kutoka katika vyanzo mbalimbali, ardhi ya kutosha ya kilimo na hali ya hewa rafiki, kuimarishwa kwa mtandao wa usafiri na usafirishaji ikiwemo ujenzi wa reli ya kisasa pamoja na huduma nyingi zinazovutia uwekezaji na biashara.

Halikadhalika Makamu wa Rais amesema Tanzania inawakaribisha wawekezaji katika sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya afya kama vile ujenzi wa viwanda vya uzalishaji wa vifaa tiba na dawa kwa kuzingatia uwepo wa soko katika ukanda nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini Mwa Afrika (SADC), kuwekeza katika kilimo, nishati,sekta ya usafiri na usafirishaji pamoja na miundombinu ya tehama.

Pia amewakaribisha kutumia vema ukuaji wa sekta ya viwanda vya ngozi ikizingatiwa Tanzania ni nchi ya pili kwa idadi kubwa ya mifugo barani Afrika. Pia amesema Tanzania ni nchi ya nne barani Afrika kwa uzalishaji mkubwa wa pamba (baada ya Mali, Burkina Faso, na Misri) na nchi ya nne kwa uzalishaji wa pamba asilia Duniani (baada ya India, China, na Uturuki). Amesema kwa sasa uwezo wa usindikaji wa pamba umeongezeka na kwa sasa zinasafirishwa nguo hadi nchini Marekani chini ya mpango wa AGOA.

Settings