Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji amelielekeza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kuongeza kasi ya utoaji wa vyeti vya Tathmini ya Athari kwa Mazingira (TAM) katika miradi inayotekelezwa nchini.
Dkt. Kijaji amesema hayo jijini Dar es Salaam wakati wa ziara ya kutembelea Ofisi za NEMC kwa ajili ya kuzungumza na Menejimenti pamoja na kufahamu majukumu ya kisheria yanayosimamia Baraza hilo.
Amesema katika kipindi hiki, Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kujipambanua katika kufungua milango kwa wawekezaji wa miradi ya maendeleo nchini, juhudi ambazo zinahitaji kuungwa mkono kwa vitendo na taasisi zote za umma ikiwemo NEMC.
“Natambua mmeendelea kufanya kazi nzuri katika kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Mazingira Sura 191…Naomba hili la vyeti vya tathimini ya mazingira tuliangalia kwa jicho la kipekee ili kuwezesha utekelezaji wa miradi” amesema Dkt. Kijaji.
Aidha Waziri Kijaji amefafanua kuwa Ofisi yake ina imani na matumaini makubwa na watendaji wa Baraza hilo katika kuakisi maono ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika usimamizi na uhifadhi endelevu wa mazingira ili kulinda afya na maisha ya Watanzania.
Ameeleza kuwa NEMC inapaswa kuwa kiungo katika kutoa ushauri wa kiufundi na kitaalamu wakati wa mchakato wa maombi ya vyeti vya tathimini ya mazingira kwa kuhakikisha waombaji wanapatiwa maelekezo ya namna bora ya kushughulikia kasoro na changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika maeneo ya miradi.
“Tunapobaini kasoro au changamoto wakati wa maombi ya vyeti tutoe msaada wa haraka ili waombaji waweze kuzirekebisha na kutoa taarifa na kuwajulisha mapema na pia tusichukue muda mrefu kwa waombaji wakisubiri huduma hii” amesema Dkt. Kijaji.
Akifafanua zaidi Dkt. Kijaji amesema Watanzania wana imani na matumaini makubwa na Baraza hilo katika usimamizi endelevu wa mazingira na hivyo kuiwezesha Tanzania kuwa na jamii salama kwa mustakabali wa vizazi vya sasa na vijavyo.
Kwa upande wake, Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Mhe. Khamis Hamza Khamis amesema Serikali itaendelea kujenga mazingira wezeshi kwa Baraza hilo ikiwemo kusimamia mchakato wa mabadiliko ya muundo wa Baraza hilo ambao upo katika hatua nzuri.
Ameongeza kuwa Baraza hilo lina wataalamu wenye ujuzi, weledi na maarifa ya kitaaluma katika usimamizi na uhifadhi wa mazingira, hivyo utaalamu huo hauna budi kutumika vyema katika kubuni na kubaini miradi inayoweza kutoa suluhisho ya changamoto za uharibifu wa mazingira nchini.
“NEMC ina wasomi wazuri wenye fani mbalimbali ambao wakitumika vyema wataisaidia nchi kuweza kupiga hatua kubwa na pia kuandaa mipango itakayosaidia kupata majibu ya changamoto za uharibifu wa mazingira katika taifa letu” amesema Mhe. Khamis.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya NEMC, Prof. Esnati Chaggu ameishukuru Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kuendelea kuiwezesha Bodi kutekeleza vyema majukumu yake kupitia Mpango Kazi ulioandaliwa na menejimenti ya baraza hilo.
Amesema katika kuharakisha kasi ya utekelezaji wa majukumu, baraza limebuni mfumo ya kieletroniki kupitia TEHAMA ambapo huduma mbalimbali zinazotolewa katika mfumo huo ikiwemo vyeti vya tathimini ya mazingira na hivyo kurahisisha utendaji kazi.
Kuhusu usimamizi wa Sheria, Prof. Chaggu amesema baraza limeendelea kusimamia utekelezaji wa sheria ya upigaji marufuku wa matumizi ya mifuko ya plastiki kwa kushirikiana na mamlaka mbalimbali za Serikali na sekta binafsi.
“Tunaishukuru Serikali kwa ushirikiano unaoipatia baraza..tunaahidi kuongeza kasi, weledi na maarifa zaidi katika kufanikisha utekelezaji wa majukumu ili tuweze kuleta tija iliyokusudiwa kwa kuzingatia maono ya Viongozi wetu” amesema Prof. Chaggu.
Aidha kwa upande Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dkt. Immaculate Sware amesema Baraza litaendelea kupokea na kutekeleza maelezo yanatolewa na Viongozi Wakuu wa Serikali katika kusimamia Sheria ya Mazingira Sura 191.
“Baraza limeendelea kufanya kazi kubwa…Tupo tayari kwa kazi na tutauwepo majini na ardhini kwani tuna wataalamu wenye weledi katika kutekeleza majukumu tuliyopewa” amesema Dkt. Sware.