Dkt. Kijaji ahimiza kasi ukamilishaji wa miradi ya Ofisi ya Makamu wa Rais

Sep, 25 2024

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji ametoa wito kwa waratibu na wasimamizi wa miradi inayoratibiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais kuikamilisha kwa wakati ili ilete manufaa kwa wananchi.

Dkt. Kijaji amesema hayo wakati wa ziara ya kukagua miradi inayoratibiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais kisiwani Pemba, Septemba 24,2024 ukiwemo Mradi wa Kuimarisha Miundombinu ya Fukwe, Sipwese, Mkoa wa Kusini pamoja na Mradi wa Jamii wa Ujenzi wa Ngazi katika Shehia ya Kizimbani, Mkoa wa Kaskazini.

Amemtaka kila mmoja kusimamia vyema eneo alilopewa ili kukamilisha kwa wakati miradi hiyo ili wananchi wanufaike nayo.

“Viongozi wetu wanatupenda ndio maana leo nimetumwa hapa ili kuangalia kinachoendelea, hivyo nitoe wito kwa wasimamizi wa miradi kuongeza kasi ya ujenzi wa miradi hii na itakapokamilika kila mmoja anao wajibu wa kuilinda,” amesema Dkt. Kijaji.

Ameongeza kuwa eneo la Sipwese ambapo linajengwa tuta la kuzuia maji ya bahari kumekuwa na mmomonyoko ambao umeanza kuleta athari katika baadhi ya maeneo kwa kusababisha uharibifu wa miundombinu iliyopo kama vile barabara, majengo, makazi ya watu na madaraja hali iliyosababisha Serikali kutumia fedha katika kukarabati miundombinu iliyoharibiwa.

Akikagua Mradi wa Utekelezaji wa Mpango wa kunusuru Kaya Maskini uliopo katika Shehia ya Kizimbani, Mhe. Dkt. Kijaji amesema madhumuni ni kuongeza kipato, fursa na uwezo wa kugharamia mahitaji muhimu, pamoja na kusaidia kujenga rasilimali watu hasa watoto kwa kuwapa elimu, huduma za afya na lishe bora.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Wete Mkoa Kaskazini Pemba, Dkt. Hamad Omar Bakari amesema walengwa wa Shehia ya Kizimbani pia wamepata mafunzo maalumu ya siku saba ya ruzuku ya uzalishaji, kuandaa mipango ya rahisi ya biashara.

Vile vile kaya zilishiriki zoezi la uhakiki wa kaya zilizoboreka kiuchumi. Kwa mwaka wa Fedha wa 2023/2024 mradi uliyotekelezwa Ujenzi wa vidaraja vya kushukia na kupandia kwa waenda kwa miguu, mradi ambao una urefu wa mita 82.

Aidha kukamilika kwa mradi huu kumewezesha wananchi ambao wanafanya shughuli zao za kilimo kufika kwa urahisi katika mashamba yao.

Settings