Dkt.Jafo: Tanzania imejiandaa kikamilifu kushiriki Mkutano wa Mabadiliko ya Tabianchi

Nov, 02 2022

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu (Muungano na Mazingira), Dkt. Selemani Jafo amesema Tanzania imejiandaa kikamilifu kushiriki Mkutano wa 27 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Kimataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi utakaofanyika Sharm El Sheikh nchini Misri kuanzia tarehe 31 Oktoba mpaka tarehe 18 Novemba 2022.

Amesema katika Mkutano wa mwaka huu, majadiliano yenye maslahi mapana kwa nchi yetu yatapewa kipaumbele na kuweka msimamo katika Malengo ya Dunia juu ya Uhimilivu wa mabadiliko ya tabianchi.

Dkt. Jafo amesema kuwa agenda ya mabadiliko ya tabianchi ndio kipaumbele cha nchi zinazoendelea na kusema kuwa umeanzishwa mkakati wa kidunia wa uhimilivu wa mabadiliko ya tabianchi. “Inakadiriwa kuwa takribani zaidi watu bilioni 3.6 wako katika hatari ya kuathiriwa na mabadiliko ya tabianchi. Hivyo, lengo la dunia kwa pamoja ni kutaka kuondokana na hali hii” Jafo alisisitiza.

Amesema masuala ya upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kukabiliana na kuhimili mabadiliko ya tabianchi yataendelea kuwa sehemu kubwa ya majadiliano kati ya nchi zilizoendelea na zinazoendelea. Amesisitiza kuwa agenda kubwa itakuwa ni upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kugharamia miradi ya mabadiliko ya tabianchi. Amesema kuwa msimamo wa Tanzania katika mkutana huo ni kutoa wito kwa nchi zilizondelea kutimiza wajibu wao ili kuwezesha uhakika na uwazi wa upatikanaji wa fedha za mabadiliko ya tabianchi.

Tanzania inasisitiza kuwekwa kwa mfuko maalum kwa ajili ya kushughulikia masuala ya hasara na uharibifu ili kusaidia nchi zinazoendelea kufanya tathmini ya kuongezeka kwa kina cha bahari na Upunguzaji wa gesijoto chini ya mkataba na makubaliano ya Paris kwa nchi zinazoendelea na kuchangia shughuli za maendeleo.

Kuhusu Masoko ya kaboni na mbinu zisizo za masoko, Dkt. Jafo amesema kuwa Msimamo wa Tanzania ni udhibiti wa matumizi ya masoko ya kaboni katika upunguzaji wa gesijoto ili kuzifanya nchi zilizoendelea kuchukua hatua za ndani kushughulikia upunguzaji wa uzalishaji wa gesijoto.

Ameyataja mambo mengine yatakayojadiliwa kuwa ni pamoja na Mfumo wa uwazi katika hatua na misaada inayotolewa kwa kuzingatia fedha za misaada zinazotolewa, kujenga uwezo na teknolojia.

“Tunasisitiza kuwa hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi zisiathiri juhudi za kijamii na kiuchumi za nchi zinazoendelea na hazipaswi kuwa njia ya ubaguzi wa kiholela, usio na sababu au kizuizi cha kujificha kwenye biashara ya kimataifa, haswa kikanda” Dkt. Jafo alisisitiza.

Settings