Dkt. Jafo awahimiza upendo wahitimu wa afya

Nov, 25 2023

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo ametoa wito kwa wahitimu wa afya kuwa na upendo kwa watakaowahudumia.

Dkt. Jafo ambae alikuwa mgeni rasmi katika mahafali ya kwanza ya Chuo cha Afya cha City College Kampasi ya Ilala amewatunuku vyeti wahitimu wa ngazi ya Diploma ya Ufamasia na Utabibu leo Novemba 25, 2023 jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na wahitimu hao amewapongeza kwa kufanya vizuri katika masomo yao na kuwataka kuwa na upendo na watakaowahudumia pindi wafanyapo kazi.

Pia, amesema watoa huduma za afya ni watu muhimu sana katika taifa na ndio maana Serikali imeendelea kutoa ajira kwa kada hiyo.

Amesema kutokana na umuhinu huo Serikali imeendelea kuimarisha miundombinu ya sekta ya afya ikiwemo ujenzi wa zahanati na hospitali ili kusogeza mbele huduma.

Amewataka wanafunzi wanaoendelea na masomo katika chuo hicho kujituma zaidi ili wanapohitimu kuwepo na wahitimu wazuri wenye kuhitajika na taifa.

Ametumia nafasi hiyo pia kuwaasa watuunze mazingira kwa kupanda miti ili kukabiliana na athari za kimazingira.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa chuo hicho Bw. Shaban Mwanga amesema City College itaendelea kuunga mkono jitihada za Serikali katika sekta ya afya kwa kutoa wahitimu bora.

Ameongeza kuwa katika mahafali hayo jumla ya wahitimu 60 wametunukiwa vyeti ambapo kati yao 18 wa fani ya Ufamasia na 42 wa Utabibu.

Settings