Habari
Masauni aitaka NEMC kuelimisha wananchi
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni ametoa wito kwa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kuendelea kutoa elimu kwa umma na wadau ili kuongeza uelewa na uzingatiaji wa Sheria ya Mazingira.
Wito huo umetolewa Septemba 18, 2026 jijini Dar es Salaam, wakati wa ziara yake Makao Makuu ya NEMC, kwa ajili ya kupokea Taarifa ya Utekelezaji wa Bodi na Uzinduzi wa Magari Mapya ya Ukaguzi na Upimaji wa Mazingira.
Pia ameitaka NEMC kuchukua hatua madhubuti za usafi wa mazingira na maandalizi dhidi ya madhara ya mvua tarajiwa za El NiNo; pamoja na kuendeleza juhudi za kudhibiti mifuko ya plastiki iliyopigwa marufuku na taka hatarishi.
Ameeleza kuwa wakati Baraza likielekea katika hatua ya kuwa Mamlaka ya Taifa ya Usimamizi wa Mazingira (NEMA), anatoa wito wa kuendelea kuimarisha maeneo mbalimbali ikiwemo marekebisho ya Kanuni za Ada na Tozo ili kuimarisha ukusanyaji wa mapato.
“Napongeza hatua za kimkakati zilizopigwa katika kipindi hiki, ikiwemo maadhimisho ya miaka 40 ya NEMC; uzinduzi wa Mfumo wa Tanzania wa Ufuatiliaji Endelevu wa Uzalishaji wa Uchafuzi (TOCEMS); kufikia asilimia 95 ya ujenzi wa Kituo cha Uelimishaji kuhusu Zebaki mkoani Geita.”
“Mazingira safi na salama ni msingi wa afya ya wananchi na maendeleo endelevu ya taifa letu. Serikali, kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais, itaendelea kuwaunga mkono ili muweze kutekeleza majukumu yenu kwa ufanisi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya NEMC Mhandisi Mwanasha Tumbo amesema Baraza linaendelea kutoa elimu ya Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira ili kuhakisha wananchi wanakua na elimu ya kutosha katika hifadhi ya Mazingira.



