Wizara yapewa maelekezo kupima maeneo ya malisho kupunguza migogoro

Nov, 04 2023

Serikali imeelekeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ipime maeneo ya malisho ya mifugo ili kupunguza migogoro kati ya wakulima na wafugaji.

Maelekezo hayo yametolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo wakati akifunga Wiki ya Maonesho ya Ufugaji wenye Tija na Utunzaji wa Mazingira kwa niaba ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Biteko jijini Dodoma.

Amesema wizara hiyo ishirikiane na TAMISEMI na Wizara ya Mifugo na Uvuvi katika kutenga maeneo ambayo yatatumiwa na wafugaji katika kulisha mifugo yao kwa utaratibu hivyo kuepuka na uharibifu wa mazingira.

Pia, Waziri Jafo ameitaka Wizara ya Maji kupitia Mamlaka za Mabonde nchini kuhakikisha yanalindwa sanjari na kusimamia zoezi la upandaji wa miti katika vyanzo vya maji ili yawasaidie wakulima na wafugaji.

“Vyuo vikuu vya kilimo na mifugo viendeleze tafiti mbalimbali za kuangalia aina ya malisho ambayo yatawasaidia wafugaji wetu kupata malisho ya uhakika kwa ajili ya mifugo,” amesema Dkt. Jafo.

Aidha, Waziri amekipongeza Chama cha Mazingira na Ufugaji Tija Tanzania (CHAMAUTA) kwa kusajili wafugaji nchini na kuwataka kuendelea na zoezi hilo ambalo litasaidia katika kuweka mfumo mzuri wa utunzaji wa mazingira.

Dkt. Jafo ambaye pia ni mlezi wa chama hicho amewapongeza kwa kuweka kipaumbele agenda ya mazingira na kusema Serikali itaendelea kuwaunga mkono.

Amewaomba wafugaji waendelee kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye amejipambanua katika uhifadhi wa mazingira hususan kupitia miradi mikubwa anayotekeleza ikiwemo inayowagusa wafugaji.

Settings