​Waziri Ummy aelekeza halmashauri ziweke miundombinu bora ya taka sokoni

Jan, 06 2021

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Ummy Mwalimu amezielekeza halmashauri zote nchini kuwa na miundombinu bora ya kukusanya, kuhifadhi na kusafirisha taka ili kulinda afya za wananchi.

Mhe. Ummy ametoa maelekezo hayo leo Januari 6, 2021 baada ya kufanya ziara ya kushtukiza katika soko la Majengo jijini Dodoma kwa lengo la kuangalia mfumo mzima wa kushughulikia taka ngumu.

Katika ziara hiyo akiwa ameambatana na watendaji kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais Idara ya Mazingira, Waziri Ummy alionesha kuridhishwa na hali ya mazingira sokoni hapo na kuipongeza halmashauri ya jiji hilo.

Akizungumza mara baada ya kukagua soko hilo alizitaka halmashauri zote nchini kuhakikisha zinatoa kandarasi kwa watu wa kukusanya na kusafirisha taka wenye vifaa bora kwa ajili ya kazi hiyo.

Waziri huyo alisisitiza kuwa kutafanyika ukaguzi wa kuona kama wakandarasi hao wana vigezo na sifa zikiwemo kuwa na vifaa vya kuwakingia watumishi wanaokusanya taka.

“Tumeona gari za kukusanya na kusafrisha taka zenyewe zikiwa ni takataka kwa hiyo tutakagua kila halmashauri wajitathmini je, kandarasi hii waliyompa mtu wa kukusanya, kuhifadhi na kusafirisha taka ana vifaa bora. Hizi ni salamu tu tunataka masoko yawe safi na salama kwa wanaouza na wateja, kikubwa tunasema mazingira safi na salama kwa ajili ya maendelevu,” alisisitiza Ummy.

Aidha, alisisitiza pawepo na utaratibu wa kuondoa taka zinazokusanywa na kuhifadhiwa kwenye masoko kwa wakati na kuwa hatavumilia kuona halmashauri yoyote ambayo takataka zinakaa kwa zaidi ya siku moja hatua itakasaidia kulinda afya za watumiaji wa masoko.

Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004 na kanuni zake inazitaka halmashauri zote za majiji, manispaa, miji na wilaya kuweka mifumo bora ya kukusanya, kuhifadhi na kusafirisha taka.

Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Mazingira na Udhibiti wa taka ngumu Jijini la Dodoma, Dickson Kimaro alisema wana changamoto ya kypotea kwa vifaa wanavyopewa vibarua na kuahidi kuendelea kutoa vifaa vifaa hivyo.

Afisa Afya wa Kata ya Majengo, Yusta Maguzu alimpongeza Waziri Ummy kwa ziara hiyo na kuahidi kuendelea kusimamia vyema mazingira katika kata yake ili kusaidia kupunguza magonjwa ya mlipuko.

Settings