Habari
Serikali kuendelea kulinda vyanzo vya maji
Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais imesema itaendelea kulinda vyanzo vya maji na mito mbalimbali nchini kwa kuzingatia Sheria ya Mazingira ya Mwaka 2004 na Sheria ya Rasilimali za Maji ya Mwaka 2009.
Pia, imesisitiza kuwa itashirikiana na Wizara ya Madini kuendelea kutoa elimu kwa wachimbaji na wananchi kwa ujumla kuzingatia sheria na taratibu ili kuwa na mazingira endelevu.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Festo Dugange bungeni jijini Dodoma leo Januari 27, 2026 wakati akijibu swali la Mbunge wa Morogoro Kusini Mhe. Zuberi Mfaume aliyetaka kujua ni hatua gani zimechukuliwa za uchafuzi wa Mto Mfizigo na Mhuva zitokanazo na shughuli za madini na kubaini kemikali zilizopo na athari zake.
Akiendelea kujibu swali hilo Mhe. Dkt. Dugange alisema mito ya Mfizigo na Mhuva iliyopo katika jimbo hilo ni moja ya maeneo ambako hufanyika shughuli za uchimbaji mdogo wa madini katika maeneo ya pembezoni mwa mito hiyo.
Alisema katika kuhakikisha mito hiyo inatunzwa na kuzuia uchafuzi wake kutokana na shughuli za uchimbaji madini, Serikali mwaka 2025 ilichukua sampuli za maji ya mito hiyo kwa ajili ya kupima ikiwa kuna uchafuzi wa kemikali zitokanazo na uchimbaji na uchenjuaji wa madini.
Dkt. Dugange alifafanua kuwa matokeo ya vipimo vya sampuli hizo vilionesha kuwa kuna kemikali za chuma na manganizi.
“Kemikali zilizobainika kuwepo zinatokana na miamba iliyo kuwa inachimbwa na sio kwamba zinatokana na matumizi ya kemikali za kuchenjulia madini kama zebaki. Aidha kemikali hizi zilibainika kutokuwa na madhara kwa binadamu na bionuwai,” alisisitiza.
Katika swali la nyongeza la Mbunge wa Kakonko Mhe. Alan Mvano aliyetaka kujua hatua za kunusuru mito, Mhe. Dugange alisema Serikali inahakikisha suala la uchimbaji linaendeshwa kwa mujibu wa Sheria ya Uhifadhi namba 191 ambapo kipaumbele ni kuweka mazingira wezeshi na utunzaji wa mazingira.



