Habari
Mpango wa Matumizi ya Maeneo ya Maji kuimarisha Uchumi wa Buluu
Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais imezindua Kikosi kazi cha Kuandaa Mpango kazi wa Kitaifa na hatua za utekelezaji wa Matumizi Endelevu ya Maeneo ya Maji (MSP) ili kuhakikisha Uchumi wa Buluu unakuwa shirikishi na kuimarika.
Kikosi hicho kimezinduliwa na Naibu Katibu Mkuu (Muungano) Ofisi ya Makamu wa Rais Bw. Abdallah Hassan Mitawi kwa niaba ya Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Richard Muyungi mjini Morogoro leo Januari, 2026.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Kikosi, Bw. Mitawi amesema Mpango kazi wa Kitaifa wa Matumizi Endelevu ya Maeneo ya Maji ni nyenzo muhimu inayotegemewa katika kuwezesha utekelezaji wa masuala ya Uchumi wa Buluu kwa kuzingatia uhifadhi wa mazingira na ustawi wa jamii.
Alisema kuwa uandaaji wa mpango unaoandaliwa kwa ushirikiano wa Serikali na Shirika la The Nature Conservative (TNC) na kazi huo ni sehemu ya jitihada za kuhakikisha Serikali inafanikiwa kupanga matumizi endelevu ya maeneo ya maji.
Bw. Mitawi alisema Sera ya Taifa ya Uchumi wa Buluu (2024) na Mkakati wake wa utekelezaji (2024 - 2034) inasisitiza kupanga matumizi ya rasilimali za maji kwa njia jumuishi na endelevu, hivyo kufanikiwa kuandaliwa kwa mpango kazi huo utasaidia katika kutekeleza majukumu ya kila kamati inayohusika kuandaa MSP kitaifa.
“Mpango kazi ni lazima kuhakikisha uratibu madhubuti wa kitaifa kuheshimu kila upande unaotumia bahari, unahitajika msikamano wa kitaasisi kuhakikisha manufaa ya bahari yanawafikia wananchi wote hivyo, MSP ni chombo cha kuimarisha rasilimali zetu za bahari na ukanda wa pwani,” alisema.
Aidha, Bw. Mitawi alisema uvuvi, usafirishaji kupitia bahari, utalii, nishati, utafiti wa kisayansi na uhifadhi wa bayoanuayi bila upangaji makini shughuli hizi zinaweza kuleta mgongano wa matumizi ikiwemo uharibifu wa mifumo ikolojia na upotevu wa fursa za kiuchumi hivyo, mpango kazi huo utakuwa ni chombo muhimu cha kusaidia kukabiliana na changamoto hizo.
Pamoja na hayo Naibu Katibu Mkuu amesema Serikali inatambua na kushukuru Shirika la TNC kwa kuwa wadau muhimu katika kuandaa mpango kazi huo wa matumzi ya rasilimali za maji kwa maendeleo endelevu.
Kwa upande waka Kaimu Meneja wa Usimamizi wa masuala ya Bahari Bw. Emmanuel Mpina kutoka TNC alisema wataendelea kushirikiana na Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais ambayo ndiyo msimamizi mkuu wa mazingira kuhakikisha kuwa sekta ya uchumi wa buluu inaendelea kuimarika
Alisema mchakato wa uandaaji wa mpango kazi huo ulianza tangu mwaka 2019 ambapo uliambatana na kufanya tathmini ya awali na namna nchi inaweza kuandaa MSP.
Hivyo, Bw. Mpina alisema matumizi ya vyanzo vya maji yakiwemo usafirishaji, utalii na uvuvi yakifanyika bila mpangilio yanaweza kusababisha kukosekana kwa fursa za maji na manufaa kwa wananchi.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Uchumi wa Buluu Ofisi ya Makamu wa Rais Bi. Finahappy Kimambo alisema mwananchi wa kawaida anaweza kunufaika na mpango kazi huo kwa kupitia shughuli anazofanya zikiwemo uvuvi na kilimo cha mwani.
Aliongeza kuwa Serikali imeamua kuandaa mpango kazi wa matumizi endelevu ya maji kwasababu kwenye bahari kama ilivyo nchi kavu kuna shughuli na wadau wakiwemo wavuvi, wasafirishaji, wachimbaji wa madini na mafuta hivyo, ili kuwa na matumizi endelevu lazima kuwe na mpango wa matumizi.
Kikosi kazi cha kuandaa Mpango kazi wa Matumizi Endelevu ya Maji na utekelezaji wake kinaundwa na wataalamu kutoka Wizara za kisekta, taasisi za serikali na wadau wa maendeleo.



