Habari
Watanzania watakiwa kupanda miti wanaposherehekea siku ya kuzaliwa
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Festo Dugange ametoa rai kwa kila Mtanzania kupanda mti angalau mmoja kila mwaka anapoadhimisha kumbukizi ya siku ya kuzaliwa ili kuleta chachu katika hifadhi endelevu ya mazingira.
Ametoa rai hiyo wakati akiongoza zoezi la upandaji wa miti kuadhimisha Kumbukizi ya Siku ya Kuzaliwa ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo Januari 27, 2026 katika Mji wa Serikali, Mtumba jijini Dodoma.
Dkt. Dugange alisema misitu ni uhai hivyo Viongozi wa ngazi mbalimbali na Watanzania kwa ujumla wanapaswa kuwa na utamaduni wa kupanda miti na kuitunza hatua itakayosaidia kuhifadhi mazingira na kukabailiana na mabadiliko ya tabianchi.
“Watanzania tupo zaidi ya watu milioni 61 kila moja wetu akiiga mfano wa Rais wetu kupanda angalau mti mmoja kila mwaka anaposherehekea siku ya kuzaliwa, tutapanda miti milioni 61 na baada ya miaka kumi tutapanda miti bilioni 61,” alisisitiza.
Akizungumzia zoezi la upandaji wa miti, Dkt. Dugange alisema ni hatua ya kuungana na Rais Dkt. Samia ambaye ni kinara katika utunzaji wa mazingira na kuwa Ofisi ya Makamu wa Rais inayo heshima ya kuungana naye kwa kumpongeza na kumtakia heri.
Naibu Waziri aliongeza kuwa zoezi la upandaji wa miti litakuwa endelevu kwa kuwa maeneo ya yanayotakiwa kupandwa miti bado yapo na miti hiyo inapatikana kwa urahisi.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Mazingira Bw. Thomas Chali alisema
pamoja na mambo mbalimbali lengo la kufanya zoezi la upandaji wa miti katika eneo hilo ni kurejesha hali nzuri ya mazingira kwa ajili ya kupumzikia.
Alisema eneo hilo lenye ukubwa wa hekta mbili ni bustani ya miti ambayo Ofisi ya Makamu wa Rais ilipatiwa mwaka 2023 na kulifanyia usafi na kuanza kupanda miti 1665 ambayo hata hivyo kutokana na ukame ni miti 982 pekee ndio ilistawi.
Hivyo, Bw. Chali alisema Ofisi imeendelea kulitunza eneo hilo la bustani kwa kushiriki kampeni za upandaji wa miti ikiwemo ya kuadhimisha Siku ya Kuzaliwa Mhe. Rais Dkt. Samia ambaye alizindua Kampeni ya Kukijanisha Dodoma alipokuwa Makamu wa Rais mwaka 2017.
Nae Kaimu Naibu Kamishna wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Dkt. Zainab Bungwa alisema inawezekana kuifanya nchi isiwe jangwa kwa kupanda miti kwa wingi.
Alisema shughuli za kibinadamu huchangia uharibifu wa mazingira na hata kutishia jangwa. Hivyo suluhisho ni kujenga mazoea ya kupanda miti badala ya kuikata.
Dk Bungwa aliongeza kuwa hadi sasa Tanzania ina jumla ya misitu 465 ambayo inamilikiwa na Serikali Kuu, Serikali za Mitaa, Vijijini na mamlaka zingine na kati ya hiyo, 26 ni hifadhi za misitu ya asili.



