​Wachimbaji wadogo waaswa kutotumia magogo kuepuka ukataji miti

Jun, 20 2021

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Hamad Hassan Chande amewataka wachimbaji wadogo wa dhahabu kutotumia magogo katika shughuli zao kwa kuwa ni chanzo cha ukataji wa miti.

Chande ametoa wito huo wakati akizungumza na wachimbaji wa mgodi mdogo wa Sekenke One uliopo wilayani Iramba Mkoa wa Singida alipofanya ziara ya kikazi ya kukagua uzingatiaji wa Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004 katika shughuli za uchimbaji.

Alisema kuwa imebainika wachimbaji wengi hukata miti kwa ajili ya kujengea mashimo lakini alitahadharisha vitendo hivyo huchangia kwa kiwango kikubwa uharibifu wa mazingira.

Aliwashauri watumie njia mbalimbali zikiwemo kujengea kwa zege mashimo hayo kwa kuwa ni salama zaidi na pia huepusha vitendo vya ukataji miti na hivyo kuendelea kuhifadhi mazingira.

“Tumekuja hapa kutembelea mgodi wenu na tumeona harakati za uzalishaji wa madini ya dhahabu lakini nitoe wito kwa wamiliki wa migodi wenye leseni tuache kukata miti na kutumia katika mashimo tutumie zege na kwa kufanya hivyo tutapunguza ukataji miti,” alisema Naibu Waziri huyo.

Pamoja na kuendelea na shughuli hizo ambazo huwaingizia kipato alitoa wito kwa wachimbaji hao kushiriki katika uhifadhi wa mazingira ikiwemo zoezi la upandaji miti na kuitunza.

Pia, Naibu Waziri huyo alisema ni vyema wakawa wanafukia mashimo baada ya kumaliza uchimbaji kwani ni chanzo cha uharibifu wa mazingira na pia yanaweza kusababisha ajali lakini.

Kwa upande wake Meneja wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Kanda ya Kati, Dkt. Franklin Rwezumula alisema Serikali imekuja na mradi wa kutoa elimu kwa wachimbaji wadogo kuhusu.

Alisema mradi huo ambao umeanza kutekelezwa utaifikia migodi midogo mbalimbali nchini ukiwemo wa Sekenke One na utakuwa na manufaa makubwa kwani utawasaidia kujifunza namna ya kufanya shughuli zao pasipo kuharibu mazingira.

Dkt. Rwezumula alisema kupitia migodi ya mfano itakayojengwa katika baadhi ya maeneo nchini wachimbaji wadogo watajifunza mbinu bora za uchenjuji wa dhahabu bila kuathiri mazingira.

Aliwataka wenye kuendesha shughuli za migodi kusajili miradi yao katika Baraza hilo kwa mujibu wa utaratibu ili zitambuliwe na kusajili hatua na kukaguliwa na kupewa cheti pamoja ushauri inapohitajika.

Pamoja na hayo aliwataka pia kuwa na utaratibu mzuri wa kuhifadhi taka za kemikali zinaztotumika katika shughuli zao hususan katika uchenjuaji badala ya kuziacha zikizagaa ovyo hali inayiweza kuhatarisha afya za wananchi wanaouzunguka migodi hiyo.

Naye Aifsa Mazingira kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, Joseph Kiwango alisema Serikali kupitia Ofisi hiyo pamoja NEMC imekuja na Mpango kazi kwa ajili ya kupunguza matumizi ya Zebaki kwa wachimnaji wadogo.

Alisema miongoni mwa shughuli zitakazotekelezwa kupitia Mpango kazi huo wa miaka mitano ni pamoja na kutoa elimu kwa wachimbaji wadogo katika migodi mbalimbali takriban 40.

Pia Kiwango aliendelea kusisitiza kuwa Serikali haijakataza matumizi wala uibngizaji wa Zebaki bali waingizaji wanapaswa kujisaili kwa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali ili kjtambulika badala ya kuingiza kinyemea.

Shughuli za uchimbaji wa madini ni miongoni mwa vyanzo vikuu vya mapato ya Taifa ambapo inaelezwa kuwa hadi kufikia Mei 2021 zaidi ya sh. bilioni 4 zilikusanywa katika mgodi mdogo wa Sekenke wilayani Iramba mkoani Singida.

Settings